Tanzania: Wakulima wa alizeti huongeza mavuno kwa kufuga nyuki

| Januari 10, 2022

Download this story

News Brief

Emiliana Lucas anaishi katika kijiji cha Kigwe wilayani Bahi, kaskazini magharibi mwa Dodoma, mji mkuu wa kiutawala wa Tanzania. Amekuwa akilima alizeti kwa takriban muongo mmoja sasa, lakini kwa miaka mitano iliyopita, faida yake imekuwa ndogo kutokana na mavuno duni. Lakini kila kitu kilibadilika mnamo 2014, wakati Bi. Lucas alipohudhuria semina kuhusu faida za ufugaji nyuki kwenye mashamba ya alizeti. Baada ya Bi. Lucas kuanza kufuga nyuki kando ya alizeti zake mwaka 2017, uzalishaji wake na faida yake iliongezeka. Alikuwa akivuna chini ya kilo 300 za mbegu za alizeti kwa hekta, lakini ameongeza mavuno yake zaidi ya mara mbili hadi kilo 620. Abdallah Mdiliko ni ofisa ugani katika eneo hilo. Anasema nyuki husaidia kuongeza uzalishaji wa alizeti kupitia uchavushaji, na kwamba nyuki ndio wachavushaji bora.

Wingu zito, jeusi linatanda polepole angani na mvua inaweza kuanza dakika yoyote. Emiliana Lucas anavuta pumzi na kutabasamu kabla ya kuweka jembe lake chini. Amekuwa akipalilia nyuma ya nyumba yake kwa karibu saa mbili sasa, tangu saa kumi na mbili asubuhi.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 36 anakimbia hadi kwenye boma lake kulisha kuku wake kabla ya kurejea kuandaa shamba lake kwa msimu ujao wa kilimo.

Bi. Lucas anasema: “Kabla ya mvua kuanza kila msimu wa kilimo, ninahakikisha kwamba shamba langu liko tayari kwa ajili ya kupanda kwa wakati. Ninapanda kwa pamoja alizeti, mahindi, mtama na kunde shambani mwangu kwa sababu mazao haya yanategemeana kwa rutuba ya udongo.”

Anaongezea, “Pia mimi hufuga nyuki katika shamba langu kwa sababu nyuki huchavusha alizeti, na pia hutoa asali.”

Bi. Lucas anaishi katika kijiji cha Kigwe wilayani Bahi, kaskazini-magharibi mwa Dodoma, mji mkuu wa kiutawala wa Tanzania. Amekuwa akilima alizeti kwa takriban muongo mmoja sasa, lakini kwa miaka mitano iliyopita, faida yake imekuwa ndogo kutokana na mavuno duni. Katika ekari moja ya ardhi, Bi. Lucas alivuna chini ya kilo 300 za alizeti.

Kila kitu kilibadilika mwaka 2014, pale ambapo Bi. Lucas alihudhuria semina ambapo alijifunza kuhusu faida za kufuga nyuki katika mashamba ya alizeti.

Bi. Lucas anakumbuka: “Mafunzo hayo yalikuwa yenye kuvutia. Ilinisaidia kuelewa idadi ya mizinga ya nyuki ninayopaswa kuwekwa kwenye shamba langu, na bajeti ambayo ningehitaji kufanya hivyo. Pia nilijifunza kuhusu aina mbalimbali za mizinga ya nyuki, na vifaa vinavyohitajika ili kuiweka katika mashamba yangu.”

Mnamo mwaka 2017, Bi. Lucas alianza kufuga nyuki kando ya alizeti zake na uzalishaji wake na faida yake iliongezeka. Mavuno yake yaliongezeka zaidi ya mara mbili kutoka kilo 300 za mbegu za alizeti kwa ekari hadi kilo 620.

Anaelezea, “Ni kwasababu ya mizinga 40 ambayo ninayo katika shamba langu la hekari 11”

Abdallah Mdiliko ni ofisa ugani katika eneo hilo. Anasema nyuki husaidia kuongeza uzalishaji wa alizeti kupitia uchavushaji na ndio wachavushaji bora.

Bw. Mdiliko anaeleza: “Kuna manufaa ya pande zote kati ya mimea ya alizeti na nyuki. Tunawahimiza wakulima kuunganisha ufugaji nyuki katika mashamba yao ya alizeti. Nyuki hufaidika kwa kupata nekta kutoka kwa alizeti, na alizeti hufaidika kwa kuchavushwa.”

Bw. Mdiliko anaongeza, “Nyuki wanavyozidi kutembelea mimea ya alizeti kutafuta chavua, ndivyo alizeti inavyozalisha zaidi. Huu ndio tunaita kufaidishana.”

Nyuki wanaweza kusaidia kuongeza uzalishaji wa mbegu za alizeti kwa asilimia 20-50. Lakini, Bw. Mdiliko anasema, hasara ni kwamba nyuki wanaweza kutengeneza utawala katika eneo karibu na alizeti.

Anaeleza, “Nyuki wanapoanza kukusanya nekta kutoka kwenye mmea huo, wangeweza kuwa na hisia ya umiliki na kujaribu kulinda mmea dhidi ya wadudu wengine, au hata wanadamu.”

Jeremiah Sobayii ni mkulima mwingine wa alizeti kijijini hapo. Anasema inasikitisha sana kwamba baadhi ya wakulima wa alizeti katika eneo lake hawana mizinga ya nyuki kwasababu wanapata hasara badala ya kupata faida.

Bw. Sobayii anaeleza, “Wakulima wanapaswa kutundika mizinga ya nyuki kwenye miti katika mashamba yao. Utaratibu huu husaidia kulinda mazingira, kuongeza mavuno, na kubadilisha mapato ya wakulima kwa gharama ya chini.

Anasema kwamba baada ya kujifunza siri za ufugaji nyuki, mavuno yake ya alizeti yaliongezeka. Sasa anawataka wakulima wengine wa alizeti kufanya ufugaji nyuki.

Bi. Lucas anasema ufugaji nyuki umemletea mabadiliko. Pesa anazopata kwa kuuza asali ni nyongeza kubwa kwa mapato yake.

Rasilimali hii inafanywa kwa msaada wa kifedha wa Wakfu wa Biovision unaotolewa kupitia mpango wa Mazoea ya Kilimo Endelevu.

Picha: Milundo ya mizinga ya nyuki. Mahali hapajulikani. Credit: Kris Fricke, 2008.