Tanzania: Kilimo mseto huongeza kipato cha mkulima

| Januari 10, 2022

Download this story

News Brief

Bwana Njelekela anaishi katika kijiji cha Lilido, katika wilaya ya Mtwara kusini mwa Tanzania karibu na mpaka wa Msumbiji. Ana shamba la ekari tatu na anatumia maji kutoka kwenye bwawa kupanda mboga mboga, matunda, na mazao kama mahindi, maharagwe na mbaazi. Anasema kuwa kilimo mseto kina faida nyingi, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mapato, usalama wa chakula, na lishe bora kwa familia yake. Kupanda mseto pia huongeza rutuba ya udongo, na kunaweza kurahisisha palizi na umwagiliaji.

Ni asubuhi nzuri ya siku ya Jumamosi na Abdulsalum Njelekela yuko shambani mwake akimwagilia mimea. Anasema, “Ninapata maji mengi kutoka kwenye bwawa karibu na shamba langu, ambayo hunisaidia kufanya kilimo cha mseto mwaka mzima.”

Bwana Njelekela anaishi katika kijiji cha Lilido, katika wilaya ya Mtwara kusini mwa Tanzania karibu na mpaka wa Msumbiji. Ana shamba la ekari tatu na anatumia maji kutoka kwenye bwawa kupanda mboga mboga, matunda, na mazao kama mahindi, maharagwe na mbaazi

Anasema: “Mahitaji ya mazao ya chakula ni makubwa katika eneo langu. Niliamua kuanza kilimo mseto ili kuzalisha zaidi kwenye kipande hicho cha ardhi na kuwauzia walaji ili kupata pesa zaidi.”

Bw. Njelekela anaongeza, “Watu katika eneo langu hununua mboga kama vile pilipili hoho, bamia na bilinganya. Kilimo mseto hunisaidia kusambaza mazao yangu kwa wateja mbalimbali.”

Anasema kwamba kilimo mseto kina manufaa mengi: “Ukulima mseto hunisaidia kupata mapato, uhakika wa chakula, na mlo wenye lishe bora kwa familia yangu. Pia inasaidia kuhifadhi mazingira kwa sababu kwa mbinu hii ya kilimo, sikati miti bali nairuhusu ikue pamoja na mazao ya chakula.”

Joseph Denis ni mkulima katika kijiji cha jirani cha Kitere ambaye amekuwa akifanya kilimo cha mseto kwa miaka miwili na anakuza mboga mbalimbali katika shamba lake la hekta moja. Anasema, “Faida ya kulima mazao mbalimbali kwa pamoja katika shamba moja ni kwamba mkulima anahakikishiwa soko la angalau moja ya mazao hayo.”

Bw. Denis anasema kuwa kilimo mseto humletea faida kubwa kuliko kupanda zao moja tu kwenye shamba lake.

Anafafanua: “Kwa sababu ya kilimo mseto, nina uhakika wa kupata kati ya shilingi 2,000,000 hadi 3,000,000 za Tanzania (Dola za Marekani 864-1,297) kwa mwaka. Ninauza kilo moja ya nyanya, hoho, au biringanya kwa shilingi 1,500 hadi 3,000 za Tanzania (Dola za Marekani 0.65-1.30).”

Anaongeza, “Kama bei ya zao moja ni ndogo sokoni, huwa sibabaiki au kuwa na wasiwasi ninaposhindwa kuuza kwasababu kwa kilimo cha mseto naweza kutegemea zao jingine.”

Bw. Denis anasema kuwa palizi na umwagiliaji ni rahisi na si kazi kubwa kwa kilimo mseto, kwani yeye hupalilia au kumwagilia mara moja tu kwa mazao mawili au matatu. Anaeleza, “Napalilia yote kwa wakati mmoja kwa mazao yote tofauti. Vile vile hutokea ninapotaka kumwagilia maji.”

Kulingana na Bw. Denis, wakulima wanaolima mseto pia huokoa pesa kwenye pembejeo kama vile dawa za kuulia wadudu kwa sababu idadi ya dawa zinazotumika hupungua.

Salma Said ni mkulima wa mboga mboga kutoka kijiji cha Lilido ambaye pia analima mseto, analima matango, nyanya chungu na bamia. Anasema, “Kutoka katika kipande kidogo cha ardhi, nina uwezo wa kuvuna mazao mbalimbali ambayo mimi hula na mume wangu na watoto wetu wawili na kisha kuuza ziada.”

Philipo Mrutu ni mtaalamu wa kilimo na biashara ya kilimo kutoka wilaya ya Morogoro nchini Tanzania. Anasema kuwa faida za kulima mazao mbalimbali katika shamba moja ni kwamba ardhi inatumika vizuri na mazao yanasaidiana au kutegemeana.

Anaongeza: “Pia inasaidia kuongeza rutuba, kwa mfano mtu anapolima na kuchunga kwa wakati mmoja, mabaki ya chakula cha mifugo yanayotumika katika kilimo tayari yana rutuba, ambayo inaweza kusaidia kilimo kustawi.

Bw. Mrutu anabainisha kuwa mazao mchanganyiko yanasaidia kutunza unyevu wa udongo na miti ikipandwa pembezoni mwa bwawa inatoa kivuli na kuboresha hali ya hewa hasa katika kipindi cha kiangazi ambacho dunia inakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Bwana Njelekela anasema kilimo mseto kimemsaidia kwa njia nyingi. Anafafanua: “Nawashauri wakulima wa eneo langu kuanza kulima mseto kwasababu kwangu nimeona faida nyingi ikiwamo mapato bora. Ninaweza kutunza familia yangu kwa sababu ya kupanda mseto.”

Rasilimali hii inafanywa kwa msaada wa kifedha wa Wakfu wa Biovision.

Picha: Mboga zinaonyeshwa kuuzwa katika soko karibu na Morogoro, Tanzania mnamo Mei 28, 2014. Credit: Sylvie Harrison.