Magnim Karouwe | Machi 26, 2024
News Brief
Akofa Amagnon ni mama wa watoto watatu ambaye aliamua kufunga duka lake kwasababu kazi zake za nyumbani zilikuwa ngumu sana. Sasa, kazi za nyumbani huchukua karibu wakati wake wote. Anaamini kwamba wanaume wanapaswa kushiriki kazi za nyumbani na kuwatambua wanawake kwa huduma isiyolipwa wanayotoa. Tchilalo Anastasie Sosso ni mwezeshaji wa mradi wa Shirika lisilo la kiserikali la Togo kuhusu unyanyasaji wa kijinsia. Bi Sosso anasema kwamba, nchini Togo, "Wanaume zaidi na zaidi, hasa wale waliosoma, huwasaidia wake zao katika kazi za kila siku. Mitazamo inabadilika polepole." Wakati huo huo, Bibi Amagnon anajikita katika kuwaelimisha watoto wake ili kuhakikisha kuwa kushiriki kazi za nyumbani kunakuwa ni desturi. Anasema, "Tayari ninamfundisha mtoto wangu mkubwa kwamba kazi za nyumbani zinapaswa kugawanywa kati ya wasichana na wavulana."
Ni asubuhi na mapema na mama wa nyumbani Akofa Amagnon anatembea kwenye njia ndogo akiwa na beseni nne tupu kichwani mwake. Bi. Amagnon anaelekea kwenye kisima cha jirani kilicho umbali wa mita 500 kutoka nyumbani kwake kuchota maji. Anaishi Elavagnon, yapata kilomita 60 kusini mwa mji wa Atakpamé nchini Togo. Anasema: “Ninahitaji kuhakikisha kwamba jagi tunalotumia kuhifadhi maji linajazwa kila asubuhi ili kutosheleza mahitaji ya kila siku ya familia yangu. Kisha, mimi hufagia ua, kuosha vyombo na kupika, na kuwasindikiza watoto wangu shuleni.”
Bi. Amagnon ameolewa na ni mama wa watoto watatu. Alikuwa akisimamia duka na ilimbidi kusawazisha kazi za nyumbani na kuendesha biashara yake. Lakini mwaka huu, aliamua kufunga duka lake kwasababu ya safari nne za kila siku anazofanya ili kuongozana na mtoto wake mdogo, ambaye ndiyo kwanza ameanza shule.
Bi. Amagnon anasema, “Sijui ni masaa mangapi kwa siku ninatumia kutunza familia yangu.” Anaongeza kwamba kazi zake za nyumbani huchukua karibu muda wake wote. Anasema, “Mimi ndiye wa kwanza kuamka na wa mwisho kwenda kulala.”
Tchilalo Anastasie Sosso ni mwezeshaji wa mradi wa Shirika lisilo la kiserikali nnchini Togo linaloshughulikia maswala ya unyanyasaji wa kijinsia. Bibi Sosso anasema kuwa kazi za wanawake zisizolipwa ni pamoja na shughuli yoyote wanayofanya kwa ajili ya utunzaji wa kaya na shughuli yoyote inayochangia ustawi wa familia kufanyika bila fidia ya kifedha. Hii inajumuisha kazi za nyumbani kama vile kutunza wanafamilia na kazi za nyumbani kama vile kupika na kuosha vyombo. Anasema kazi hizi za nyumbani zimekabidhiwa kwa wanawake pekee nchini Togo kutokana na mawazo ya awali kutoka kwa elimu ya jadi. Anasema, “Tangu wakiwa wadogo, wasichana hufundishwa kupika, si wavulana.”
Bi Amagnon anatumaini kuwa juhudi zake ambazo hazijalipwa zitatambuliwa. Anaamini kwamba wanaume wanapaswa kuwasaidia wake zao kwa kazi kama vile kuwapeleka watoto shuleni, na kwamba wanapaswa kuwatambua na kuwatia moyo wanawake kwa matunzo yote wanayotoa kwa ajili ya ustawi wa familia.
Alika Passenda ni mwalimu katika shule ya sekondari ya Elavagnon CEG na anaishi katika kitongoji cha Kossi Kope. Anakubali kwamba mke wake ana jukumu kubwa katika kuendesha nyumba. Anasema yeye hushughulikia kazi za nyumbani, akimuachia wakati wa majukumu yake ya kikazi. Lakini mara nyingi humsaidia mke wake kwa kuwaogesha watoto au kuwatunza pale mke wake akiwa na shughuli nyingi jikoni.
Bibi Sosso anasema kuwa wanaume wanaweza kuchangia katika kutambua thamani ya kazi za nyumbani za wanawake, lakini kwamba hii inahitaji kuongeza ufahamu kuhusu jinsi wanandoa wanaweza kushiriki kazi za nyumbani. Shirika lake lisilo la Kiserikali linaendelea kuelimisha wanaume kusaidia wanawake zaidi, na wanaona maendeleo fulani. Anasema, “Wanaume wengi zaidi, hasa wale waliosoma, huwasaidia wake zao katika kazi za kila siku. Mitazamo inabadilika polepole.”
Bi Sosso anasema kuwa kazi za wanawake ambazo hazijalipwa hazizingatiwi na hazitambuliki katika familia licha ya mchango wake muhimu katika utendaji kazi na ustawi wa familia. Anakadiria thamani ya kifedha ya kazi isiyolipwa ya mwanamke nchini Togo kati ya 10,000 FCFA na 40,000 FCFA ($16 hadi $66 za Marekani) kwa mwezi.
Anaeleza: “Huu ni wastani wa mshahara wa wasaidizi wa nyumbani. Kiasi hiki ni kidogo kwa sababu sio kazi zote zinazozingatiwa. Vitu vingine haviwezi wekewa gharama, kama vile kutunza wanafamilia.”
Anaongeza kuwa utafiti wa NGO ulikadiria kuwa mama mlezi wa nyumbani hutumia hadi saa 20 kwa wiki kufanya kazi za nyumbani ikilinganishwa na saa 12 kwa wanaume.
Bibi Sosso pia anaamini kuwa wanawake wanaoacha kazi zao za kitaaluma ili kutunza familia wanapaswa kusajiliwa katika mfuko wa hifadhi ya jamii ili wanufaike na pensheni ya kustaafu.
Wakati huo huo, Bi. Amagnon analenga katika kuwaelimisha watoto wake ili kuhakikisha kuwa kushiriki kazi za nyumbani kunakuwa ni desturi. Anasema, “Tayari ninamfundisha mwanangu mkubwa kwamba kazi za nyumbani zinapaswa kugawanywa kati ya wasichana na wavulana.
Rasilimali hii imeandaliwa kupitia mpango wa ‘UCARE – Unpaid Care in sub-Saharan Africa‘, ambao inalenga kuongeza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kupitia dhamira ya kugawana zaidi haki na usawa wa matunzo yasiyolipwa na kazi za nyumbani ndani ya kaya na familia katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano wa Farm Radio International (FRI), UN Women, na The African Women’s Development and Communications Network (FEMNET) kutokana na ufadhili wa Global Affairs Canada.