Tanzania: Wafugaji hutumia taarifa za hali ya hewa kupanga malisho ya mifugo

| Febuari 4, 2020

Download this story

Peter Kakanji anapiga mswaki kwa kutumia kijiti kilichotafunwa vizuri mithili ya mswaki. Anatazama angani kuona dalili za mvua za karibuni kwa sababu usiku uliotangulia alisikia redioni kwamba mvua itanyesha leo. Anasema “mvua imeanza mapema mwaka huu na bado inanyesha maeneo mbali mbali ya nchi kadiri ya utabiri wa hali ya hewa ulivyotangazwa redioni”.

Bwana Kakanji ni mfugaji anayeishi kijiji cha Mairowa kilichoko wilaya ya Longido kiasi cha kilometa 90 kaskazini mwa Arusha katika ukanda wa kaskazini mwa Tanzania. Anamiliki mbuzi 150, kondoo 120 na ng’ombe 80 lakini malisho si ya kutosha.

Madhara ya kuhamahama na mifugo kutafuta malisho ni pamoja na maambukizo ya magonjwa na upotevu wa mifugo. Kuepuka matatizo haya Bwana Kakanji anatumia vizuri taarifa za utabiri wa hali ya hewa katika kufanya maamuzi kama vile wakati ufaao kutenga eneo la kutosha kwa malisho kwa mifugo yake.

Kama ilivyo kwa wafugaji wengine katika eneo lake, Bwana Kakanji hupata taarifa za utabiri wa hali ya hewa kutoka mamlaka ya hali ya hewa Tanzania kupitia simu yake ya kiganjani na pia kupitia kituo cha redio ya kijamii kiitwacho Orkonerei Radio Service (ORS).

Bwana Kakanji anasema kwamba ukilinganisha na matangazo ya kawaida ya hali ya hewa, taarifa anazopata kupitia hii radio ya kijamii (ORS) na kupitia whatsApp ni ya kina zaidi. Maafisa ugani hutoa mwongozo kuhusu mvua na kupendekeza shughuli bora za kilimo na ushauri kuhusu muda wa kuandaa mashamba na mbegu bora za kupanda.

Anasema “kimkakati Taarifa hizo pia hushauri wafugaji hasa wale wafugaji wanaoishi maisha ya kuhama kuhusu njia bora za kulisha mifugo yao kwa mzunguko”.

Kwa mujibu wa Bwana Kakanji, mvuakatika eneo lao zinapungua kila mwaka jambo linalosababisha upungufu wa malisho na maji ya kunywesha mifugo. Upungufu wa mvua hulazimu wafugaji kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Lakini kwa kutumia taarifa za utabiri wa hali ya hewa kwa sasa wanaweza kubashiri wapi wanaweza kupata maji na malisho.

Kwa miongo kadhaa sasa Bwana Kakanji na familia yake ya watu 14 wamekuwa wakitumia njia ya jadi ya kuchunga na kuhama na mifugo kutoka sehemu moja kwenda nyingine kutafuta maeneo ya kutosha kuchunga mifugo. Mabadiliko haya ya kiwango na majira ya mvua yameigharimu sana familia ya Bwana Kakanji wakati wanahamahama.

Kuhamahama huku mara nyingi huchukua miezi miwili hadi mitatu. Katika nyakati hizi wafugaji huacha familia zao katika makazi yao ya kudumu. Bwana Kakanji anasema kitu kibaya zaidi ni kwamba wakati wa kuhamahama huku wanapoteza ng’ombe wengi kutokana na magonjwa ambayo huyapata katika maeneo mapya ya malisho wanayohamia.

Anasema “mbung’o ni tatizo kubwa ambalo hatujaweza kukabiliana nalo kwa mafanikio”.

Fulla Yassin ni afisa ugani katika wilaya ya Longido. Anasema kwamba wafugaji ambao wamepata taarifa za utabiri wa halia ya hewa kupitia simu zao za kiganjani wananufaika na taarifa zinazotolewa kwa wakati ambazo huwawezesha kujua wapi na lini mvua zitanyesha. Bwana Yassin anasema kwamba taarifa za hali ya hewa kupitia redio zinawasaidia pia kupanga vizuri matumizi ya chakula na maji kwa ajili ya ng’ombe wao.

Kipindi cha redio hutangazwa kwa dakika 30 siku ya Ijumaa saa tatu usiku na kurudiwa siku ya Jumamosi saa 12.30 jioni. Anaongeza kwamba “taarifa za redio na zile za whatsapp hutolewa kwa lugha ya Kiswahili na Kimaasai ili kuwezesha wafugaji wengi kuelewa kwa urahisi taarifa hizo japo bado kuna masuala yenye mawasiliano duni”.

Mbali na whatsapp na vipindi vya redio, Bwana Yassin anasema kwamba wafugaji wanatumia kitumizi cha simu za mkononi kiitwacho Afriscount kilichobuniwa kuwawezesha wafugaji kujua ramani za malisho ya kuchangia katika maeneo yao.

Anaendelea kusema “inawasaidia pia kufanya maamuzi sahihi zaidi na yenye kuokoa gharama yanayohusu kuhama, uboreshaji wa malisho na ushirikiano, kupungua hatari ya upotevu wa mifugo na hatimaye kuboresha maisha yao.”

Rahel Oleselea ni mjane na mama wa watoto sita na wajukuu wane, na ni mfugaji katika kijiji cha Oletesi katika wilaya ya Longido. Anasema kwamba upatikanaji rahisi wa taarifa za hali ya hewa kupitia redio na simu za viganjani inamsaidia kupanga kiasi cha chakula anahitaji kununua kwa ajili ya ng’ombe wake.

Anaelezea “Nilikuwa napanga kuongeza na kuhifadhi malisho mengi zaidi kwa ajili ya ngombe wangu kabla mvua haijanyesha, lakini mpango huu haupo tena. Ninapata taarifa kwamba mvua itanyesha na tulishauriwa kuanza kurudi katika makazi yetu ya kudumu tukiwa na mifugo yetu”.

Taarifa za hali ya hewa na hasa utabiri unaotolewa kila misimu hutoa msingi wa matunzo yenye tija kwa mifugo kwa sababu wachungaji wanaweza kubashiri maeneo yatakayokuwa na malisho na maji katika muda mahususi wa mwaka.

Bwana Kakanji anasema amenufaika kikubwa na taarifa za hali ya hewa hasa anapokuwa anafanya maamuzi ya mahali pa kupeleka mifugo wake kwa ajili ya malisho.

Anaelezea “Wakati wa kiangazi, huwa tunahamia eneo la ardhi ya Jeshi liliko Ongorika ambalo halitumiki kwa makazi wala kwa kilimo. Wakati malisho yanapopungua tunahamia Ngorika hadi Mwita maeneo yaliyoko Monduli kupitia vijiji vya Esilalei, Naitorya, na Msakini.”

Jarida hili limeandaliwa kwa ufadhili wa Shirika la Chakula Duniani kupitia mradi wa Kufikisha taarifa za hali ya hewa kwa wakulima na wafugaji.