Neema Joseph | Mei 7, 2018
Ni majira ya saa mbili asubuhi. Akiwa amefunga kitenge cha rangi ya blue na nyekundu kiunoni, Lucia Shiwa anachuchumaa shambani kwake kukagua shamba lake la tikiti maji. Anasema, “Hii ni kazi yangu … tuna hakikisha mashamba yanakaguliwa kabla hatujaendelea na majukumu mengine.”
Bi. Shiwa ni mama wa miaka 38 mwenye watoto tisa. Anaishi katika kijiji cha Nyakabare, umbali wa kilimeta 30 kutokea mji wa Geita uliopo kaskazini magharini mwa Tanzania. Mara nyingi asubuhi huwa anatembea umbali wa kilometa nne kutoka nyumbani kwake kwenda katika shamba lake lenye ukubwa wa hekari tatu ambapo analima mboga, tikiti na matunda mengine.
Baada ya kutafuta kazi kwa muda wa miaka nane bila mafanikio, Bi. Shiwa aliamua kujiunga na wanachama wengine mwaka 2006 na kuunda kikundi cha Environmental Group. Lengo lao lilikuwa ni kuongeza shughuli zao za kilimo kwa kulima pamoja na kilimo binafsi. Anaelezea, “Kupitia kilimo cha [pamoja] tumeweza kufanya biashara ya kulima kwa pamoja na kupata kipato ambacho kimetuboreshea maisha yetu.”
Katika kikundi wakulima wanazalisha na kuuza mboga mboga na matunda kama nyanya, karoti, spinachi, kabichi, zucchini, maharage machanga, tikiti maji, na matango.
Bi. Shiwa anaelezea kikundi kinatoa ajira kwa wanawake na vijana. Anaelezea sasa ni rahisi kwa wakulima kupata misaada ya kifedha na mafunzo kutoka kwa mashirika binafsi nay a kiserikali.
Bi. Shiwa anasema kuwa watu wanaotaka kujifunza kuhusu kilimo wanavutiwa kujiunga na kikundi kwasababu ya fursa za mafunzo zilizopo katika kikundi. Anaongeza, “Tuna mashamba darasa ambapo tunawapatia mafunzo wakulima wengine.”
Anasema kampuni za mbegu zimetoa mafunzo. Wanakikundi wamejifunza jinsi ya kuandaa udongo, matumizi ya viuatilifu, na kupanda kwa nafasi ili kuboresha mavuno. Anasema, “Sasa tunapanda matango kwa umbali wa sentimita 20 kutoka mstari mmoja hadi mstari mwingine na sentimita 10 kutoka mmea mmoja hadi mmea mwingine.”
Masunga Daniel ni kijana wa miaka 18 mkulima wa tikiti maji na ni mwanakikundi kutoka Nyakabare. Anasema, “Kilimo ni fursa kwa vijana wasio na ajira. Nina lima kama biashara kama biashara nyinginezo, ijapokuwa sio rahisi.”
Kwa mfano, Bw. Daniel anaelezea, kufikisha mazao sokoni ni moja ya changamoto kubwa kwao: “Hakuna magari katika kijiji cha Nyakabare. Maranyingine tunalazimika kutumia pikipiki na baisikeli kupeleka mazao mijini, kutafuta masoko.”
Pamoja na mavuno mabaya msimu uliopita, Bw. Daniel na wanakikundi wenzake wanaendela kulima wakiamini kuwa kazi zao ngumu siku moja zitawalipa. Anasema, “Sio kazi rahisi kuwashawishi vijana kujiunga na kilimo. Wengi wao wanaamini kuwa kilimo ni kazi za watu masikini.”
Hamis Mchenye ni katibu wa kikundi cha Environmental Group. Anawahimiza wanawake na vijana wasio na ajira waanze kuzalisha matunda na mboga mboga. Anasema, kuuza kwa pamoja kunawawezesha wakulima kuwez kuuza mazao mengi zaidi. Lakini kikundi bado kina jitahidi kutafuta wanunuzi na kupata bei nzuri.
Bw. Mchenye anaongeza: “Ni vigumu kupata masoko. Mara nyingine tunauza mazao yetu kwa bei ndogo sana. Hatuna namna lakini inatubidi tu kuuza [kwasababu] hatuwezi kuacha mzao yakaoza shambani.”
Ijapokuwa ukosefu wa masoko inabakia kuwa changamoto kubwa, kikundi cha wakulima kiliweza kumuunganisha Bi. Shiwa na mnunuzi wa tikiti maji. Anauza tikiti maji zake katika mgodi wa madini Geita kwa shilingi 3,000 kwa tikikiti moja (sawa na dola 1.30) hii ni bei ya reja reja, na kwa bei ya jumla anauza kilo moja kwa shilingi 750 (sawa na dola 0.33).
Mwaka jana, Bi. Shiwa alaiwekeza shilingi 800,000 (sawa na dola 350), kwa kununua mbegu, mbolea na vibarua ili aweze kulima heka moja la matunda. Alivuna tani nne za matunda na kuuza kwa shilingi 3,200,000 (sawa na dola 1,400).
Hela alizopata kwa kuuza matunda na mboga, Bi. Shiwa alijenga nyumba ya bati na kulipa ada za watoto wake. Anamatumaini ya kuweza kuwahimiza wanawake na vijana katika eneo lake kuchukulia kilimo kama shughuli za kibiashara.
Uniterra Tanzania inafanya kazi na mashirika ya ndani katika sekta ya matunda na mbogamboga na utalii wa ndani kuwasaidia vijana na wanawake kupata fursa za kiuchumi. Uniterra imewezesha malipo ya makala hii. Uniterra inapokea misaada ya kifedha kutoka serikali ya Canada, inayowafikia kwa kupitia Global Affairs Canada, www.international.gc.ca. Jifunze zaidi kuhusu Uniterra Tanzania katika Facebook katika tovuti hii: facebook.com/wusctanzania