Tanzania: Kukosekana soko la kueleweka la soyalishe kumewavunja moyo wakulima

| Juni 19, 2017

Download this story

Utiga ni kijiji kidogo kilichopo mkoa wa Njombe nchini Tanzania, umbali wa zaidi ya kilomita 700 kutoka Dar es salaam karibu na mpaka wa nchi za Zambia na Malawi. Kijiji hiki kipo nyanda za juu kusini nchini Tanzania, ambako wakulima wengi wanazalisha soyalishe.

Daniel Lungo ni mkulima mdogo anayelima soyalishe, lakini anahangaika kupata bei nzuri jambo linalomkatisha tamaa kuongeza uzalishaji. Wakulima wa eneo hili wamekuwa wakishauriwa kuwekeza kwenye uzalishaji wa zao hili la soya hata hivyo wamekuwa wakiuza mazao yao kwa bei ya chini licha ya uhitaji mkubwa wa soya katika makampuni mbalimbali yanayozalisha chakula cha binadamu na wanyama.

Bwa. Lungo anaeleza “Changamoto inayotukabili ni ya bei. Wafanyabiashara wanafurahia kwa kujipangia bei kandamizi kwenye soya yetu. Mfanyabiashara anapendekeza bei za chini ukilinganisha na gharama za uzalishaji, wanafanya hivi pasipo kuzingatia wakulima wametaabika kiasi gani na gharama tulizotumia tangu kulima hadi kuvuna.”

Wakulima mara nyingi wanaona kama wanalazimishwa kukubaliana na bei ndogo inayotolewa na madalali ambao baadaye huenda kuiuza bidhaa hiyo kwa bei yenye faida kubwa. Bw. Lungo anasema alitumia sh40,000 sawa na Dola 17.70 kuandaaa shamba lake na gharama zingine za manunuzi ya mbegu, mbolea na dawa za wadudu kama sh100,000 sawa na dola 44.

Ili kupata bei nzuri Bw. Lungo aliamua kusafirisha mazao yake hadi kwenye soko ambako madalali huuzia na katika kusafirisha magunia 60 ya soya kwa bus umbali wa kilomita 500 kutoka Njombe hadi morogoro ilimgharimu kiasi cha sh300,000 sawa na dola 133. Huko aliuza kila gunia kwa sh35,000, ambapo baada ya kutoa gharama alipata faida ya sh460,000 sawa na dola 204.

Anasema “Ni rahisi zaidi kusafirisha mzigo kwa njia ya mabasi kuliko kutumia malori ya kukodisha kutoka Njombe hadi sokoni.”

Wakati Bw. Lungo akitia bidii kubwa kuuza soya yake, wakulima wenzake wamejita zaidi katika uzalisha mdogo wa matumizi ya nyumbani kwa sababu hawadhani kuwa soya inafaida.

Bw. Frank Mwagike ni baba wa watoto kumi anayelima shamba umbali wa kilomita 60 kutoka Njombe mjini. Bwana huyu mwenye umri wa miaka 56 amekuwa akilima soya kwa zaidi ya miaka 15, lakini tatizo la soko limemfanya aendelee kulima soya katika vishamba vidogo vidogo tu.

Bw.Mwagike anasema alipoanza kulima soya mwaka 2001 kwenye eneo dogo ilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani tu. Hakuweza kupata soko la soya ya ziada aliyoizalisha. Anasema “Nilikaa na soya yangu ndani kwa zaidi ya hata miezi mitatu pasipo kupata mnunuzi.

Lakini baada ya shirika lisilo la kiserikali katika eneo hilo limeendelea kuwahamasisha wakulima kulima zaidi soya kwa ajili ya biashara na Bw. Mwangike sasa anazalisha soya katika shamba la ukubwa wa robo tatu heka.

Shirika lisilo la kiserikali la Farm Input Promotions Africa (FIPS) linasaidia wakulima wa soya mkoani Njombe kuongeza uzalishaji. Deo Msemwa yeye ni meneja uendeshaji na anasema wakati mwingine uzalishaji wa wakulima ni mdogo jambo ambalo linawafanya wanunuzi kuelekea sehemu nyingine ambako wanaweza kupata bidhaa hiyo kwa wingi kulingana na mahitaji yao.

Moja ya wanunuzi hao wakubwa ni kampuni ya Highlands ya Iringa wanatengeneza unga wa lishe kwa ajili ya uji. Wanunuzi wengine wakubwa ni pamoja na Silver Lands ya Iringa na Tanfeed ya Morogoro. Wanunuzi hawa hutumia bidhaa hii kutengeneza chakula kwa ajili ya matumizi ya binadamu na kuku.

Bw. Msemwa anasema, “Mahitaji kwa mwaka kwa wanunuzi wa soya ni zaidi ya tani 100 wakati uzalishaji wa wakulima wetu ni chini ya tani kumi na hivyo mkulima hawezi kulalamika kuwa hakuna soko.”

Uzalishaji wa ndani ni mdogo sana na hivyo soya imekuwa ikiingizwa kutoka nchi za Zambia na kwingineko.

Bw. Geoffrey Israel Kirenga ni Mtendaji Mkuu wa Mpango wa kuendeleza kilimo nyanda za juu Kusini (SAGCOT) yeye anabainisha kuwa “Nyanda za juu kusini peke yake wanauwezo wa kuzalisha hadi tani miliomi mbili za soya ingawa kwa sasa wanazalisha kiasi kidogo sana”. Hivyo anashauri ipo haja ya kuwekeza zaidi kwenye uzalishaji wa soya hapa nchini ili kukidhi soko la ndani na kuzui uingizaji wa soya toka nje ya nchi.

FIPS inahamasisha wakulima kuongeza uzalishaji kwa njia mbalimbali ikiwemo kuwapa habari juu ya njia mbalimbali za uzalishaji, utumiaji wa mbegu bora zinazokinzana na magonjwa na kutoa mazao mengi. Pia wanaweza kuongeza nguvu ya soko kwa kuungana kwenye vikundi na kuuza pamoja kwani upatikanaji wa bidhaa nyingi pamoja kunaweza kuvutia wanunuzi na bei nzuri.

Salome Kanyunyu ni miongoni mwa wakulima wengi waliohamasishwa na shirika la FIPS kuwekeza kwenye kilimo cha soya ili kujiongezea kipato. Bi. Kinyunyu mama wa miaka 38 anayelima kijiji cha Litundu anasema, “Nilisita sita sana kuanza kulima zao hili kwa sababu wakulima walioanza kulima awali walituambia halina soko, ila nilianza kulima bada ya kutiwa moyo na FIPS baada ya kutuambia soko lipo.”

This work was carried out with the aid of a grant from the International Development Research Centre, Ottawa, Canada, www.idrc.ca, and with financial support from the Government of Canada, provided through Global Affairs Canada, www.international.gc.ca