Lovemore Khomo | Juni 10, 2020
News Brief
Malawi, serikali inashauri watu kukaa umbali wa angalau mita moja kutoka mtu mmoja hadi mwingine, waache kushikana mikono, kuepuka mikusanyiko ya watu zaidi ya 100, na kupunguza idadi ya watu katika gari za umma na za binafsi. Harusi na huduma za kidini zimepigwa marufuku. Serikali ilitangaza kuwa masoko yangefunguliwa kwa nusu-siku, lakini hili imepingwa katika mahakama, na halijatekelezwa. Watu lazima wazingatie hatua za kutotangamana katika masoko, lakini hawazingatii hatua hizi. Bi Maganga anasema kuwa hatua za udhibiti wa COVID-19 zimebadilisha jinsi wakulima wanauza bidhaa zao, kwa sababu uuzaji kwa wateja unahitaji kukaribiana na hata kugusana. Anaongeza: “Hatua za kudhibiti "COVID-19 zimefunga ufikiaji wa masoko, jambo ambalo litapunguza mapato yetu kutokana na kilimo. Nategemea masoko ya hapa kuuza nyanya zangu na viazi ulaya ili kuhudumia familia yangu."
Ni mchana uliotulia, siku yenye ubaridi na Ida Maganga anafika nyumbani kutoka katika shamba lake la viazi na nyanya lililopo takribani mita 200 kutoka nyumbani kwake. Mama huyu wa miaka 35 mwenye watoto watatu anaonekana kutatanishwa na kukosa furaha. Hivi karibuni, wateja wanaonunua mazao yake hawaji tena kwa idadi kubwa kufanya manunuzi katika eneo lake.
Bi Maganga anasema hii ni kwa sababu ya hatua za kutotangamana kwa wanajamii ambazo serikali ilitangaza hivi karibuni ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19). Hii inamaanisha kwamba anahitaji haraka kujua njia za kuuza mazao yake yanayoweza kuharibika.
Anasema, “Kuja kwa ugonjwa wa virusi vya corona kutalemaza bei ambayo tayari sio nzuri ya viazi ulaya na nyanya katika soko. Hii itapunguza sana mapato yangu. “
Bi Maganga analima katika kijiji cha Kapenuka, wilaya ya Dedza, kama kilomita 90 kusini mwa Lilongwe, mji mkuu wa Malawi. Alisikia kwanza juu ya COVID-19 kwenye redio na baadaye kupitia taarifa ya angalizo kwenye simu kutoka kwa Wizara ya Afya.
Anasema, “Nilijifunza kuwa ishara na dalili za mtu aliyeambukizwa virusi vya corona ni kukohoa, kupiga chafya na homa.”
Anaongeza: “Walakini, niliogopa pale niliposikia habari kuhusu hatua za kutotangamana zinazowekwa na serikali ili kuhakikisha kuwa watu wachache wanaambukizwa. Nilijua kwamba hii ingeniathiri vibaya mimi kama mkulima. “
Malawi, serikali inashauri watu kukaa umbali wa angalau mita moja kutoka mtu mmoja hadi mwingine, waache kushikana mikono, kuepuka mikusanyiko ya watu zaidi ya 100, na kupunguza idadi ya watu katika gari za umma na za binafsi. Harusi na huduma za kidini zimepigwa marufuku.
Serikali ilitangaza kuwa masoko yangefunguliwa kwa nusu-siku, lakini hili imepingwa katika mahakama, na halijatekelezwa. Watu lazima wazingatie hatua za kutotangamana katika masoko, lakini hawazingatii hatua hizi.
Bi Maganga anasema kuwa hatua za udhibiti wa COVID-19 zimebadilisha jinsi wakulima wanauza bidhaa zao, kwa sababu uuzaji kwa wateja unahitaji kukaribiana na hata kugusana. Anaongeza: “Hatua za kudhibiti “COVID-19 zimefunga ufikiaji wa masoko, jambo ambalo litapunguza mapato yetu kutokana na kilimo. Nategemea masoko ya hapa kuuza nyanya zangu na viazi ulaya ili kuhudumia familia yangu.”
Oliver Enock ni mfanyabiashara mwanamke ambaye hununua nyanya kwa bei ya jumla kwenye shamba na kuuza kwa wachuuzi katika masoko ya ndani. Yeye ni mama wa watoto wawili na anaishi katika kijiji cha Nkungumbe wilayani Dedza.
Anasema hatua za kudhibiti virusi vya corona ni mauaji ya biashara yake. Pamoja na hatua za kutotangamana, wachuuzi wengi wanaonunua nyanya na viazi ulaya vyake, wanaona ni ngumu kusimamia usafirishaji kwa sababu ni watu wachache wanaoruhusiwa kwenye gari moja.
Anaongezea: “Kabla ya ugonjwa huo, nilikuwa nikinunua vikapu vitano vya nyanya kwa siku kwa wakulima na nilikuwa nikipata faida ya Kwacha 5,000 za Malawi sawa na dola 6.70 za kimarekani ($ 6.70 US). Kwa hatua za kutotangamana zilizopo sasa, ninaweza kununua vikapu vitatu vya nyanya kwa siku, ambayo nipate faida ya karibu kwacha 3,000 za Malawi ambayo ni sawa na dola 4 za kimarekani ($ 4 US).”
Richard Nguluwe ni muuzaji wa samaki mwenye umri wa miaka 29 kutoka kijiji cha Ntchetche wilayani Lilongwe vijijini. Anasema hatua za kutotangamana zimepunguza faida yake ya kila siku kutoka karibu kwacha 8,000 za Malawi sawa na dola 10.70 za Kimarekani ($ 10.70 US) hadi karibu kwacha 3,000 za Malawi ambazo ni sawa na dola 4 za Kimarekani ($ 4 US).
Bwana Nguluwe anaelezea: “Ninaelewa ugonjwa wa virusi vya corona ni mbaya na ninajaribu kufuata hatua za kutotangamana. Lakini hii imeathiri maisha yangu ya kila siku kwa sababu biashara yangu ya samaki imekwama. Nategemea samaki kutoka ziwani na ikiwa hatua hizi za kujikinga na COVID-19 zitafuatwa, nitapata wapi samaki na nitauza kwa nani?”
Chisomo Botha ni afisa ugani wilayani Dedza. Anasema kwamba ingawa hatua kama vile kutotangamana kwa watu zinaathiri vibaya mapato ya wakulima kutokana na kupungua kwa shughuli za soko, ni muhimu sana kwa wakulima kufuata hatua za kupambana na virusi.
Bwana Botha anaelezea: “Nyanya, kabichi, karanga, na mahindi yote hutoka vijijini na husambazwa katika miji. Kwa hivyo ni muhimu kwetu kushirikishana habari na wakulima ili kuwasaidia wasieneze au kuambukizwa COVID-19 kwa sababu wakulima wapo katikati na ndio chanzo kikuu cha chakula kwa watu ambao wanaishi katika miji na majiji. ”
Ingawa mapato ya Bi Maganga yamepungua, anasema ataendelea kufuata hatua za kutotangamana ili kujilinda yeye na familia yake, ingawa itakuwa na athari ya muda mrefu kwa kiwango chake cha maisha.
Anaelezea: “Mpango wangu mwaka huu ulikuwa kukarabati nyumba yangu kwa kutumia mapato kutoka kwenye kilimo, lakini kwa bei mbaya na ukosefu wa wateja, faida yangu itakuwa kidogo na ninalazimika kungojea wakati mzuri zaidi wakati hatua za kutotangamana zitakapoondolewa ili kufanikisha ndoto zangu. “
Rasilimali hii imeandaliwa kwa msaada wa kifedha kutoka kwa serikali ya Canada uliotolewa kupitia Global Affairs Canada.