Zambia: Hela inakuwa kwenye miti kwahiyo msiikate (IPS)

| Aprili 24, 2020

Download this story

Jennifer Handondo amesimama na kikundi cha wakulima wakiangalia mashamba yao na kutafakari. Lakini yeye hafikirii kuhusu mazao ya chakula ambayo yeye amepanda lakini anafikiria haswa kuhusu miti. Bi Handondo ni mkulima mdogo katika wilaya ya Choma kusini mwa Zambia. Anahimiza miti kama chanzo kizuri cha mapato ya ziada kwa familia za wakulima.

Mama huyu ambaye ametalikiwa, hulea peke yake watoto wake watatu. Lakini kutokana na hali ya joto kuwa juu na mvua kuwa ya kiwango kidogo, imepelekea kupata mavuno machache tofauti na alivyotarajia. Kwa hivyo aliamua kuanza shughuli nyingine ya kujiingizia kipato kwa kuuza mbegu za Mwarobaini, Moringa pamoja na miti mingine ya dawa.

Bi Handondo anasema, “Kwangu, miti inawakilisha pesa na maisha, lakini sio kwa njia mbaya kama kupitia uzalishaji wa mkaa, lakini kupitia miche hii.” Anaongeza pia thamani kwa kutengeneza poda kutoka kwenye majani ya moringa, ambayo ni chakula kilichothibitishwa na pia ni mti wa dawa.

Bi Handondo hupata wastani wa karibu dola 78 za Kimarekani kila mwezi kutokana na kuuza miche ya miti na poda. Lakini anapopata oda kubwa ya poda ya moringa huweza kujipatia dola za kimarekani 5,400 kwa mwezi. Taasisi kubwa hutoa oda hizi kubwa na Bi Handondo hutegemea msaada wa wakulima wengine ili kukamilisha oda hizi.

Zambia ina eneo kubwa la misitu. Misitu inawakilisha karibu 66% ya eneo lote la ardhi na kuna aina ya miti 220 ndani ya nchi. Walakini, bioanuwai hii tajiri iko hatarini kutoweka kutokana na ukataji miti, ambayo hupunguza kiwango cha misitu kwa kiwango cha hekta 300,000 kwa mwaka.

Kulingana na mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira ya Zambia, ukataji wa miti unasababishwa na sababu kadhaa, ikijumuisha ukataji haramu wa miti, ukataji wa miti bila kujali, ukataji wa miti usio stahiki kwa ajili ya kuni, mkaa na uvunaji wa mbao. Misitu pia hupotea pale ambapo miti hukatwa kwa ajili ya kusafisha ardhi kubwa ya kilimo au kwa ajili ya kukua kwa mji na uanzishwaji wa makazi mapya ya binadamu.

Bi Handondo anapenda sana miti, na amekuwa akishiriki katika kampeni za upandaji miti na programu za uhamasishaji tangu mwaka 2016. Sasa ni wakala wa mabadiliko na kiongozi wa mradi wa uvumbuzi wa asili unaosimamiwa na World Vision Zambia.

Kisiki Hai (Farmer-managed natural regeneration – FMNR), inajumuisha kukuza upya miti na vichaka kutoka katika mashina yaliyokatwa, kutoka katika mizizi au kutoka kwenye mbegu na lengo likiwa ni kurudisha katika hali nzuri shamba lililoharibika pamoja na rutuba ya udongo.

Bi mandondo anaongezea: “Tuna vichaka vingi ambavyo vimedorora na ambavyo havikui kwasababu vimesongamana, lakini tulipopunguza matawi kupitia njia ya Kisiki Hai, tumeona kwamba hivi vichaka vinakuwa na kuwa miti, na kuunda msitu unaohitajika kwa sana, kwasababu ushindani wa kutumia virutubisho kutoka kwenye udongo unakuwa umepunguzwa.”

Kisiki Hai inakusudia kuongeza thamani na idadi ya mimea yenye miti kwenye shamba. Kusudi lingine kuu ni kuwezesha jamii kupata maarifa ili kupunguza ukataji miti.

Shadrick Phiri ni mtaalamu wa kilimo na rasilimali asili anayefanya kazi na World Vision Zambia. Anasema kwamba, Kisiki Hai (FMNR) inaweza kufanywa na wakulima binafsi au na jamii, na inaweza kuzingatia usimamizi wa miti katika maeneo ya misitu iliyolindwa au kwenye ardhi ya malisho.

Bwana Phiri anasema mradi wa World Vision unajumuisha wakulima 600 ambao wanafanya Kisiki Hai (FMNR) katika mkoa wa kusini mwa Zambia na kaya 2,600 kote nchini.

Mradi wa World Vision ni moja tu ya juhudi nyingi za kukuza shughuli za upandaji tena wa miti na kurejesha ardhi zilizoharibika nchini Zambia. World Wildlife Fund for Nature, Bio Carbon Partners, Benki ya Dunia, Umoja wa Mataifa na wakala wa Usimamizi wa Mazingira wa Zambia (Zambia Environmental Management Agency) wote wanaongoza au kuunga mkono juhudi zao binafsi.

Jukumu la wakulima na jamii za wenyeji katika kupunguza ukataji miti ilikuwa mada muhimu ya majadiliano katika Jukwaa la Mazingira Ulimwenguni (Global Landscape Forum) yaliyofanyika Ujerumani mnamo mwezi Juni. Mkutano huo uliangazia ushahidi kwamba kutambua kihalali mamlaka ya jamii juu ya misitu yao na ardhi yao husababisha kupungua kwa viwango vya ukataji miti. Hii ndio sababu Kisiki Hai (FMNR) inalenga uongozi wa jadi kama washirika muhimu.

Bwana Phiri anaongezea, Kama wasimamizi wa ardhi kubwa ya kitamaduni ambapo shughuli nyingi za ukataji miti hufanyika, tunaamini kuhusika kwao ni muhimu sana katika kurekebisha uharibifu.”

Tyson Hamamba ni mwakilishi wa Chief Choongo kutoka Mkoa wa Kusini. Kwenye mkutano na jamii mapema mwaka huu, alipendekeza viongozi wa jadi wapewe nguvu zaidi chini ya Sheria ya Kijiji ili kushughulika na wakosaji wanaokata miti. Bwana Hamamba alisema hii ndio njia pekee ya kuzuia uchomaji mkaa na uchomaji moto wa misitu wa makusudi na tabia zingine za uharibifu.

Simulizi hii imechukuliwa kutoka katika Makala iliyochapishwa na Interpress News Service na ilipewa kichwa cha habariori, “Hela inakuwa kwenye miti – Msiikate.” Kusoma nakala yote, nenda kwenye tovuti: http://www.ipsnews.net/2019/07/money-grows-on-trees-dont-uproot/

Toleo la Kiswahili la jarida hili limeandaliwa kwa ufadhili wa Justdiggit kupitia mradi wake wa Kisiki Hai (Farmer Managed Natural Regeneration – FMNR) ulioko mjini Dodoma.