Emmy Daniel Ojara | Novemba 23, 2020
News Brief
Nchini Uganda, akina mama wajawazito wanapata shida kwasababu vizuizi kutokana na COVID-19 kumefanya upatikanaji wa huduma za afya ya mama na uzazi iwe ngumu zaidi. Milly Apiyo ni mama wa miaka 25 na mmojawapo ambaye hivi karibuni alipoteza mtoto wake ambaye bado alikuwa hajazaliwa katika mwezi wa tisa wa ujauzito kutokana na kuwa hakuwa na uwezo wa kusafiri kwenda hospitali ya mkoa. Wakati wa janga hili, gharama ya usafiri wa umma iliongezeka mara tatu. Bi Apiyo alikuwa na shida na alishauriwa na madaktari katika kituo cha afya kilicho karibu kwamba angehitaji kusafiri kilomita 50 kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Gulu au ahatarishe kupoteza mtoto wake.
Milly Apiyo anatokwa na machozi wakati akijitahidi kuelezea jinsi hivi karibuni alivyompoteza mtoto wake ambaye hajazaliwa kwasababu hakuweza kufika kwenye kituo cha huduma ya afya.
Alipoteza mtoto kwasababu familia yake haikuweza kukusanya pesa kwa ajili ya usafiri wa umma, ambayo imeongezeka mara tatu kwa sababu ya hatua za kuzuia COVID-19. Anasema, “Siwezi kuamini kwamba amekufa, mtoto wangu ambaye hajazaliwa na mtoto wa kwanza wa kiume.”
Bi Apiyo ni mama wa miaka 25 ambaye anaishi katika kijiji cha Parokia ya Oroko katika wilaya ya Gulu nchini Uganda. Yeye ni mkulima mdogo na mumewe ni mlemavu.
Mwishoni mwa mwezi Julai, alimpoteza mtoto wake ambaye hajazaliwa mwezi wa tisa wa ujauzito baada ya kupata shida katika uzazi, hali ambayo madaktari walielezea kama kifo cha kichanga ndani ya tumbo la uzazi (intrauterine fetal death – IUFD).
Bi Apiyo alikuwa na maumivu ya mara kwa mara chini ya tumbo na tumbo la uzazi siku moja kabla ya kumpoteza mtoto ambaye alikuwa bado hajazaliwa.
Anaelezea: “Nilitafuta matibabu katika Kituo cha Afya cha kilichopo karibu, kituo cha Oroko III, karibu kilomita nne kutoka nyumbani kwangu. Madaktari walinishauri kusafiri kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Gulu katika jiji la Gulu, karibu kilomita 50, kwa uangalizi wa haraka-au nitahatarisha kumpoteza mtoto ambaye bado hajazaliwa. ”
Lakini familia ya Bi Apiyo haikuweza kukusanya pesa kumudu usafiri kufuatia kuongezeka kwa nauli kutokana na COVID-19.
Anaelezea: “Nauli ya usafiri wa umma kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Gulu ni shilingi 60,000 za Uganda ($ 16.06 US). Nauli imeongezeka mara tatu kwa sababu ya janga la COVID-19. Serikali pia ilitangaza kwamba kila gari inapaswa kubeba nusu ya uwezo wake. “
Anaongezea: “Tulijitahidi kujaribu kukusanya pesa lakini tulishindwa kwasababu biashara zetu ndogo ziliacha kufanya kazi kwasababu ya athari zile zile za COVID-19. Pamoja na mume wangu, tulijaribu kuomba msaada kutoka kwa jamaa na marafiki ambao wanaishi katika maeneo ya mjini. Lakini pia walisema kwamba hawakuwa na pesa kwasababu biashara zao zililemazwa na janga la COVID-19. “
Akiwa hana uwezekano wa kupata huduma za afya katika hospitali ya mbali, Bi Apiyo alirudi siku iliyofuata Kituo cha Afya cha Oroko III akiwa na maumivu makali.
Ili kuokoa maisha yake na ya mtoto ambaye hajazaliwa, wafanyikazi katika kituo hicho waliomba gari la wagonjwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Gulu. Lakini ilikuwa imechelewa sana. Alianza kutokwa na damu na hakuna mtu aliyeweza kumhudumia katika gari la wagonjwa.
Anasema: “Nadhani barabara mbaya ilichangia sana kusababisha maumivu yangu na kupoteza damu. Gari ya wagonjwa ilisafiri zaidi ya masaa saba hadi kufika kwenye kituo, lakini nilikuwa nimetokwa na damu nyingi na nilijua kuwa kuna jambo halikuwa sawa. “
Wakati gari la wagonjwa lilipofika hospitalini, Bi Apiyo alikuwa karibu amepoteza fahamu. Wauguzi walimkimbiza kwenye wodi ya uzazi.
Madaktari walisema mtoto ambaye hajazaliwa alikufa kwasababu ya kutokwa na damu nyingi na shida kwa kichanga. Bi Apiyo anasema: “Ni jambo la kuumiza sana kwangu lakini najua Mungu ana neno juu ya kila kitu. Janga la COVID-19 halijanyima riziki yangu tu, lakini pia limechangia kifo cha mtoto wangu. ”
Anaongeza: “Mara kadhaa nilikosa ukaguzi wa ujauzito na ukaguzi wa mara kwa mara kwasababu ya ukosefu wa usafiri kwenda kwenye vituo vya afya. Wakati wowote nilipokuwa mgonjwa, nilikuwa nikinunua dawa za kutuliza maumivu katika duka la karibu la dawa, nikifikiri kwamba yote yatakuwa sawa.”
Uchunguzi wa kabla ya kujifungua ni muhimu na Shirika la Afya Ulimwenguni linapendekeza angalau uchunguzi mara nne.
Daktari Christine Akidi Susan ndiye anayesimamia wodi ya uzazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Gulu. Anasema kuwa, kwakuwa serikali iliweka vizuizi nchi nzima kwasababu ya janga la COVID-19 mnamo mwezi Machi, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Gulu inasajili angalau visa 16 vya vifo vya watoto ndani ya tumbo la uzazi na wakati wa kujifungua kila wiki.
Dk. Akidi anasema: “Kupigwa marufuku kwa usafiri wa umma na kuongezeka kwa nauli za usafirishaji kwasababu ya COVID-19 kumewalazimisha akina mama wajawazito kutumia dawa za kujitafutia na kutafuta msaada kutoka kwa wakunga wa jadi. Hii imeweka maisha yao na ya watoto wao ambao bado hawajazaliwa hatarini.”
Ili kuepusha au kupunguza aina ya matukio kama ambalo Bi Apiyo alipata, Dk Akidi anasema kwamba, kwa kushirikiana na kikosi kazi cha COVID-19, hospitali sasa inatekeleza vitendo kadhaa ili kusaidia wanawake wajawazito.
Anaelezea: “Katika mikoa tofauti, tumeanzisha uhamasishaji mkubwa wa jamii juu ya afya ya uzazi, ufikiaji wa jamii, na magari ya wagonjwa yaliyo tayari kukabiliana na dharura. Tunapendekeza pia uchunguzi wa mara kwa mara wa akina mama wajawazito.”
Rasilimali hii imeandaliwa kwa msaada wa kifedha kutoka kwa serikali ya Canada uliotolewa kupitia Global Affairs Canada.