Tanzania: Wakulima hutumia mifuko ya plastiki na mapipa kuhifadhi mahindi yasishambuliwe na wadudu waharibifu

| Aprili 8, 2019

Download this storyNi adhuhuri, Rose Alexander anaendelea kufagia kwenye chumba anachotumia kuuhifadhi mahindi yake. Bibi Alexander anasema, “Ninajitahidi kila wakati kuweka katika hali ya usafi chumba ninachohifadhia mahindi, ninaweka mahindi yangu kwenye mifuko ya plastiki na mapipa ili kuzuia mahindi yasishambuliwe na wadudu.”

Bi Alexander anaishi katika kijiji cha Maroroni kilichopoMkoa wa Arusha kaskazini mwa Tanzania. Ili kuzuia upotevu kutokana na wadudu wakati wa kuhifadhi, bibi hyuyo huhifadhi mahindi yake kwenye mapipa na kwenye mifuko ya plastiki ambayo wadudu hushindwa kupenya kirahisi.

Wakulima wengi hupoteza mavuno ya nafaka wakati wa kuhifadhi kutokana na mbinu mbovu za usafirishaji na utunzajiwa nafaka baada ya kuvuna, kwa mfano, kutohakikisha kuwa mahindi yamekauka vizuri au hayana wadudu. Bi Alexander pia alikuwa aking’oa mmea mzima ili uweze kukauka shambani kabla ya kusafirisha kwenda kuhifadhi, kitendo ambacho hupelekea nafaka kushambuliwa na wadudu waharibifu.

Anavuna magunia kama 50 ya mahindi yenye kilo 100 kwa kila gunia kwa mwaka mzima kutoka kwenye shamba la ekari tano. Lakini, hadi alipoanza kutumia mifuko ya plastiki na mapipa katika kuhifadhi mahindi yake, alikuwa akipoteza kiasi cha kilo 50 za mahindi kutoka kwenye kila mfuko kutokana na kushambuliwa na wadudu kama fukusi na dumuzi.

Kabla ya mwaka 2017, alikua akitumia magunia ya kawaida kuhifadhi mahindi yake. Lakini, wadudu waliweza kuingia kwa urahisi kwenye magunia hayo na kusababisha hasara kubwa.

Bi Alexander anasema, “Wadudu walikuwa wakishambulia mahindi, tulikuwa na wasiwasi mkubwa, lakini alikuja afisa ugani kutufundisha jinsi ya kupunguza upotevu wa mahindi baada ya kuyavuna kwa kutumia mifuko ya plastiki na mapipa.”

Kufuatia ushauri wa afisa ugani huyo, Bi Alexander alinunua pipa kubwa la plastiki la lita 200 lenye uwezo wa kuhifadhi kilo 100 za mahindi.

Honest Mseri ni mkulima kutoka wilaya ya Meru ambaye pia hutumia mifuko ya plastiki na mapipa katika kuhifadhi mahindi yake. Anasema kuwa, ingawa kutumia vyombo vya plastiki kunasaidia wakulima kupunguza sana upotevu wa mazao baada ya kuvuna, bado gharama ya vyombo hivyo ni kubwa.

Honest Mseri anasema inagharimu kiasi cha shilingi 2,300 za kitanzania ambazo ni sawa na dola moja (1) ya kimarekani kununua mfuko wa plastiki wenye tabaka mbili-mfuko wa kilo 50- au kilo 100 ndani ya mwingine Pipa la plastiki hugharimu shilingi 30,000 za kitanzania sawa na dola 15 za kimarekani.

Maneno Chidege ni mtafiti mwandamizi katika Taasisi ya utafiti wa viuatilifu vya wadudu wa kitropiki kilichopo jijini Arusha. Anasema kuwa wakulima wanakabiliwa na changamoto kubwa wakati wa kuhifadhi mahindi yao, na kwamba kushindwa kuhifadhi mahindi yao kwa usalama ni mojawapo ya sababu za upotevu mkubwa wa mavuno unaosababishwa na wadudu waharibifu.

Bwana Chidege anasema wakulima wanapaswa kuhakikisha kuwa mahindi yao yamekauka vizuri kabla ya kuhifadhi. Unyevu mwingi husababisha kuoza. Pia, anapendekeza kuwa wakulima watumie mifuko ya plastiki yenye tabaka mbili katika kuhifadhi mahindi ili kudhibiti wadudu.

Bi Alexander anasema mifuko ya plastiki na mapipa imemsaidia kupunguza upotevu wa mahindi yake kutokana na wadudu waharibifu. Kwa sababu ya teknolojia hii ya plastiki, familia yake sasa ina chakula cha kutosha. Anasema, “Mahindi ni chanzo kikubwa cha chakula kwetu, Tunauza ziada inayopatikana na kupata ada za shule na pia nilipata mtaji wa kuanzisha biashara ndogo.”

Hadithi hii imeandaliwa kwa ufadhili wa The Rockefeller Foundation kupitia programu yake ya YieldWise.