Tanzania: Wakulima hutumia njia za asili na viatilifu katika kuthibiti wadudu wanaoshambulia mahindi

September 24, 2019
A translation for this article is available in French English

Ni msimu wa mvua katika wilaya ya Karagwe, na mkulima mkongwe wa miaka 58 Jane Joseph amesimama katika shamba lake la mahindi, akiwa anashanga kwa nini mahindi yake hayakui vizuri. Anainama na kuangalia baadhi ya majani ya mahindi na kugundua uwepo wa dumuzi kwenye mmea.

Bibi Joseph anasema “Hawa wadudu ni matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi. Ukame na joto limesababisha kuongezeka kwa wadud hao. Tunalima mahindi mengi, lakini wadudu hao wameharibu karibu mahindi yetu yote, iliyopelekea hasara kubwa.” Anasema kua viwavijeshi huanguka na kula mashina ya mahindi na kukaa ndani ya shina na kujificha.

Karagwe ni moja ya eneo majawapo Tanzania ambalo huzalisha mahindi kwa kiasi kikubwa. Katika siku za karibuni eneo hilo limevamiwa na viwavijeshi, hali iliyopelekea kupungua kwa mavuno na njaa mnamo mwaka 2016 na 2017. Wakulima katika eneo hili wametumia njia mbali mbali katika kupambana na viwavijeshi na wadudu wengine ikiwemo njia za kiasili na viatilifu. Lakini njia hizo zote zimefeli. Hakuna njia iliyotoa matokeo ya uhakika na njia zote zinaleta ugumu katika matumizi au kiasi sahihi na bei sahihi.

Protas Patrice ni mwenyekiti wa kijiji cha Katanda. Alipoulizwa ni wadudu gani anaowajua alisema “Najua wadudu hao kwa majina ya kilugha chetu cha kinyambo. Wanaitwa mtobere na kamshokweine. Hawa ni wadudu wadogo wadogo ambao wanatambaa na kula mashina. Wamesababisha uharibifu mkubwa hapa kijijini kiasi kwamba wakulima kama mia tatu hivi wamekata tama na kilimo cha mahindi.”

Bwana Patrice anasema hajawahi kutumia viatilifu kwa sababu ni gharama kubwa. “Siwezi kutumia 50,000 tsh (dola 22 za Marekani) kununua dawa, na hata ukinunua hiyo dawa haitoshi kunyunyuzia shamba lote.”

Catherine Kungya anaishi katika kata ya Kihanga na amekua akilima maisha yake yote. Analima mahindi, maharage, ndizi na kahawa kwenye heka moja ya shamba lake. Bibi Kaungya anasema kwamba, Siku hizi wakulima wengi wanatumia majivu and udongo kuzuia wadudu kushambukia mazao yao. Yeye mwenyewe anachanganya majivu na udongo pamoja na kunyunyiza mchanganyiko huo katika shina la mmea. Anasema kunaasaidia, lakini ni ngumu kutengeneza mchanganyiko unaotosha kutumia kwenye shamba lote.

Cleophance Kanjagaile ni Afisa Ugani kutoka wilaya ya Karagwe. Anasema ongezeko la idadi ya wadudu ambao wanashambulia mahinndi ni matokea ya joto kali. Amesema kwamba wadudu wamekua wakila shina na kijiwekea uzio kujilinda na dawa yeyote ambayo itakua inaweza kuwaua.

Ameshauri kua wakulima watumie madawa ya viwandani kuthibiti wadudu waharibifu. Anasema: “Wakulima wengi wanatumia mchanganyiko wa majivu na udongo kuthibiti wadudu waharibifu lakini njia hii sio ya uhakika. Inabidi wakulima watumie viatilifu katika kuua wadudu. Ni garama kidogo lakini viatilifu ni vya uhakika na humsaidia mkulima kupata mavuno mazuri kwa kuzuia wadudu kuathiri mazao yake.”

Lakini, kama ilivyo tiba asili, viatilifu vinafanya kazi kwa usahihi endapo yatatumiwa kiusahihi- na hata kama yakitumiwa kwa usahihi pia yanaweza yasiuue wadudu wote. Avit Theophil ni mkulima mwingine kutoka katika wilaya ya Karagwe. Anasema kwamba wengi wao waliotumia hayo madawa wanalalamika kua mazao yao yanakua kama yana kutu katika mashina na matawi hata kama mkulima anafuata maelekezo katika vibandiko au lebo. Anashauri kua, “Wataalamu wanahitaji kutafuta viatilifu vitakayofanya kazi kwa uhakika.”

Magdalena William ni mtaalam wa mbegu katika Kituo cha utafiti Maruku, Tanzania. Anasema kwamba ni muhimu kukumbuka kua mafanikio ya kutumia viuatilifu kupambana na viwavijeshi na wadudu kunategemea sababu nne. Moja, kemikali maalumu iliyotumika. Kemikali husika inakua na matokea mazuri kwa wadudu fulani lakini isifanye kazi kwa wadudu wengine. Pili, muda wa kutumia. Ni vizuri kutumia viuatilifu kuaangamiza viwavijeshi asubuhi na mapema ama jioni kabisa. Tatu, mchanganyiko uliotumika. Wakulima mara zote wanashauriwa kufuata maelekezo yaliyopo kwenye vibebeo ili kuelewa ni mchanganyiko kiasi gani unapaswa kutumika. Na mwisho, viuatilifu vinafanya kazi kwa ubora sana kulingana na hatua za ukuaji wa viwavijeshi. Ni rahisi sana kumudu viwavijeshi vikiwa vidogo kuliko vikubwa.

Wakulima waliopo magharibi mwa Tanzania hawajazoea kuzungumza juu ya namna ya kuzuia wadudu wanaoathiri mahindi katika mashamba yao. Ni mpaka mtaalamu aseme ama atoe muongozo namna ya kusthibiti viwavijeshi na wadudu wangine, kukuza mahindi kunaweza kua kugumu na kwenye mashaka kuliko ilivyo kawaida.

Taarifa hizi zimeletwa kwenu kwa msaada wa AGRA, Muungano wa Mapinduzi ya Kijani Afrika kupita mradi shirikishi wa “Kuongeza kipato na uhakika wa chakula kwa wakulima Magharibi mwa Tanzania/Karagwe”. Hata hivyo, sio lazima kua maoni yaliyowasilishwa kwenye kijarida hiki ni maoni ya AGRA au shirika linguine lolote.