- Barza Wire - https://wire.farmradio.fm -

Maswali na Majibu (Q&A) na mwandishi wa Kitanzania Koleta Makulwa, mshindi wa uandishi habari za kisayansi

Koleta Makulwa ni mwandishi wa habari za udadisi na muandaaji na mtangazaji wa vipindi vya redio katika kituo cha redio cha Radio Free Afrika mkoani Mwanza, ameshinda tuzo ya kimataifa ya uandishi wa habari za kisayansi mwaka 2017 kutoka katika jopo la wazi la majadiliano juu ya kilimo cha bioteknolojia Barani Afrika (OFAB). Katika mahojiano haya na Barza Wire, Bi. Makulwa anatushirikisha baathi ya manufaa na changamoto za uandishi wa habari ambao tayari amekuwa akiufanya kwa muda wa miaka 10.

Nini kilikuvutia kufanya kazi za uandishi kama ajira?

Nilivutiwa kufanya kazi ya uandishi wa habari kama ajira kwasababu tangu nikiwa mdogo nilikuwa naipenda kazi ya uandishi pia mimi ni mtunzi wa mashairi nilikuwa nikitunga mashairi shuleni kwahiyo naipenda kazi ya uandishi wa habari kwakuwa inaenda sambamba na kipaji changu.

Changamoto gani kubwa umewahi kukutana nazo kama muandishi?

Nimekutana na changamoto ya kukosa ushirikiano kutoka kwa authorities hasa wakati wa kutoa balance story. Pia nakosa support kutoka kwa muajiri wangu ili kuwafikia watu wasio na sauti (voiceless people) ambao ndio wahitaji wakubwa wa waandishi kufikisha kero zao kwa mamlaka husika. Mara nyingi huwa najigharamia kwenda vijijini kuwafikia voiceless na kuibua changamoto zao kwenye sekta ya kilimo na afya.

Kwa Tanzania, kuna wasichana wacheche wanafanya kazi za uandishi kulinganisha na wanaume, kwanini?

Wasichana wengi wanasoma uandishi lakini hawaifanyi kama ajira kwa sababu uandishi wa habari ni wito huwezi kufanya kazi hii kama hujitoi kwa maana kazi hii inataka mtu anaeweza kutoa muda wake na pesa yake kwaajili ya wengine. Wasichana wengi hubadili kazi kwasababu ya changamoto za uandishi wa habari ikiwemo upatikanaji wa vyanzo vya habari na namna ya kuibua mambo mapya yatakayoleta mjadala na kupatiwa ufumbuzi. Wasichana wengi hupenda kufanya kazi studio kutangaza hawapendi kwenda field.

Nini kinakupa motisha kuendelea kuifanya hii kazi?

Kinachonipa motisha kuendelea kuifanya hii kazi ya uandishi wa habari ni kwasababu naipenda pia naendelea kwasababu nimekuwa mchango mkubwa kufikisha changamoto za wasiosikika na kutatuliwa changamoto zao. Kwa mfano niliwahi kufanya habari ya uchunguzi kwenye kiwanda cha tumbaku morogoro kulikuwa na wafanyakazi walioathirika wakiwa kazini wakanyimwa haki zao niliweza kuwasaidia kupaza sauti zao kupata haki.

Ni kitu gani muhimu umejifunza kama mwandishi?

Kitu muhimu nilichojifunza kama mwandishi ni kuwa karibu na wahitaji. Ninapozunguka vijijini wakulima wanafurahi kufikiwa moja kwa moja na kusikilizwa kuliko kukaa mjini na kuripoti habari za warsha na semina. Nimegundua watu wa vijijini wanahitaji waandishi wa habari zaidi kuliko watu wa mjini. Mimi nimeamua kujitoa kwaajili ya voiceless people nakujiweka sawa na wao ili nipate taarifa na kuzifikisha kwa authorities.

Unaweza kuelezea wakati ambapo uliona vipindi vya redio yenu vinamatokeo kwa jamii?

Wakati wa magonjwa ya mahindi na mihogo niliiona matokeo ya vipindi vyangu kupitia radio yangu. Wakulima walipewa elimu ya kupambana na magonjwa pia vipindi vyangu vya kilimo viliweza kuwaunganisha maafisa kilimo na wakulima. Nilijisikia vizuri sana kuona kipindi changu kimeweza kutatua changamoto za wakulima.

Kipindi cha Koleta Makulwa kinaitwa Inuka. Kipindi kinarushwa redioni kila siku ya Jumapili saa moja jioni Redio Free Afrika, Mwanza. Radio Free Afrika ni mdau wa shirika la Farm Radio International.