- Barza Wire - https://wire.farmradio.fm -

Uganda: Marufuku katika masoko ya mifugo kwasababu ya Virusi vya Corona (COVID-19) hufanya maisha kuwa magumu kwa mfugaji wa kuku

Ni saa sita kamili mchana katika siku ambayo ina hali ya joto kutokana na jua, na hali ya joto inaongezeka hadi digrii 30 Nyuzi joto lakini Geoffrey Komakech yuko kutingwa na kazi akiezeka nyumba kwa ajili ya kujipatia kipato cha ziada. Bwana Komakech anaishi katika kijiji cha Latwong, kaunti ndogo ya Awach, katika wilaya ya Gulu kaskazini mwa Uganda.

Mfugaji huyu wa kuku mwenye umri wa miaka 40 anasema, “Hivi sasa, ninakuza kuku wa nyama aina ya broila takribani 200 na ninatumaini kuwa nitapata nafasi ya kuziuza.” Lakini vizuizi katika masoko ya mifugo kwasababu ya Virusi vya Corona (COVID-19) imebadilisha kila kitu na Bwana Komakech ana wasiwasi juu ya kipato chake.

Anasema: “Kipato changu kimepungua kwasababu ya marufuku katika masoko ya mifugo kutokana na Virusi vya Corona (Covid – 19) kwasababu watu ambao walikuwa wananunua kutoka kwangu wote wameacha kununua kuku. Hii inaathiri kipato changu ambacho ninakitumia kusaidia familia yangu.”

Mnamo tarehe 22 Machi, Serikali ya Uganda ilitangaza kwamba, kudhibiti kuenea kwa Virusi vya Corona (COVID-19), ambavyo vilikuwa vimeambukiza watu 53 nchini kwa wakati huo, ingekataza mikusanyiko yote ya umma, masoko ya mifugo, mahudhurio ya shule, na mifumo ya usafirishaji. Marufuku hiyo ilianzishwa kwa muda wa mwezi mmoja, lakini bado muda umeongezwa. Mifugo sasa inaweza kuuzwa katika mashamba ambayo mifugo hiyo inakuzwa/inafugwa.

Kwa kulinganisha, katikati mwa Aprili, masoko ya chakula nchini Uganda yalikuwa bado wazi, ingawa wachuuzi na wateja walikuwa wakiambiwa kukaa umbali wa mita nne. Usafiri wote wa umma na wa binafsi nchini umesimamishwa isipokuwa huduma za dharura, usalama, usafirishaji wa mizigo, na misamaha mingine michache.

Marufuku ya masoko ya mifugo ni ngumu kwa wafugaji wa kuku kama Bwana Komakech. Anaelezea, “Kabla ya janga la Virusi vya Corona, siku yangu ya kazi ilikuwa ikianza saa mbili kamili asubuhi. Kwa kawaida nilianza kwa kupiga simu kwa ajili ya mawasiliano ya biashara yangu.”

Anaongeza: “Kila siku, nilikuwa nikipeleka kuku kumi kwa wateja wangu na nilikuwa nikipata takribani shilingi 100,000 za Uganda (dola 26 za Kimarekani). Fedha hii ilikuwa ikinisaidia kulipa ada ya shule kwa watoto wangu sita.”

Lakini kwasababu masoko ya mifugo sasa yamepigwa marufuku, Bwana Komakech hawezi kuuza kuku kwa wateja wake. Wateja wake wengi ni wachuuzi, na kutokana na kuzuka kwa Virusi vya Corona (COVID-19), yeye hauzi kuku yoyote.

Alikuwa akitengeneza kipato kizuri. Anaelezea: “Kulisha kuku 200 hunigharimu kiasi cha shilingi 1,400,000 za Uganda (dola 369 za Kimarekani) kwa kipindi cha mwezi mmoja na siku kumi. Baada ya kuuza kuku wote, nilikuwa nikipata faida ya karibu shilingi 600,000 za Uganda (dola 157 za Kimarekani) [kila mwezi na siku 10].

Obalim Charles ni afisa mifugo wilayani Gulu. Anasema kuwa, ingawa masoko ya mifugo yamepigwa marufuku, bado wakulima wanaweza kuuza mifugo yao kwenye mashamba yao, au kuwasilisha moja kwa moja kwa wateja. Bwana Charles anafafanua kuwa masoko mengi ya mifugo yamejaa watu na hayana vifaa vya kusafisha mikono, jambo ambalo ni hatari kwa kuenea kwa Viruzi vya Corona (COVID-19).

Dk. Ruth Aceng ni Waziri wa Afya wa Uganda. Anasema kuwa hatua kama vile marufuku katika soko la mifugo inathibitisha kuwa njia bora ya kuzuia maambukizi ya Virusi vya Corona (COVID-19). Dk. Aceng anaongeza, “Bila kizuizi au hatua za watu kukaa/kusimama mbali kutoka mtu mmoja hadi mwingine, janga lingekuwa limefika mbali.”

Kiasano Olanya ni mfugaji na mwenyekiti wa Chama cha Wachinjaji wa Mifugo Wilaya ya Gulu. Anasema, “Tulikuwa tunachinja ng’ombe 20 kwa siku kwa ajili ya kuuza kwenye mabucha yetu lakini sasa tunachinja na kuuza kati ya ng’ombe sita hadi kumi kwa siku.”

Bwana Olanya anasema kuwa, kutokana na marufuku ya masoko ya mifugo, hawezi kusafiri umbali mrefu kununua ng’ombe wa kuuza, kwahiyo hununua mifugo kutoka katika mashamba ya karibu.

Wateja wa Bwana Komakech huuza kuku katika migahawa midogo pembeni ya barabara katika mji wa Gulu. Lakini biashara zao zimepigwa marufuku kudhibiti kuenea kwa Virusi vya Corona (COVID-19), na sasa Bwana Komakech hana wateja.

Anasema hataacha kukuza kuku kwasababu ya marufuku ya Virusi vya Corona (COVID-19), lakini atapunguza gharama zake za ufugaji. Anapanga kuanza kutengeneza lishe yake mwenyewe ya kuku. Hivi sasa, kuku wake wote huwafuga katika mfumo huria, ambao hupunguza gharama zake za kuwalisha.

Rasilimali hii inafanywa kwa msaada wa kifedha wa Serikali ya Canada iliyotolewa kupitia Mambo ya Kimataifa Canada.