- Barza Wire - https://wire.farmradio.fm -

Tanzania: Wanawake wakulima watafuta mikopo nafuu kuongeza uzalishaji wa mihogo

Ni majira ya saa saba mchana, ambapo nimefika katika kijiji cha Kongo kilichopo Bagamoyo, mkoani kilometa 60 kutoka jiji la Dar es Salaam, mji mkuu wa kibiashara nchini. Mariam Katema akibeba jembe begani akiwa katika barabara ya vumbi anaelekea katika shamba lake la mihogo. Baada ya kukagua mihogo yake, mwanamama huyu wa umri wa miaka 59 anaelezea jinsi ya kuvuna muhogo uliokomaa, akishika shina kwa mkono mmoja huku akitingisha na kuvuta mti wa muhogo juu, shina zima lenye mihogo linang’ooka.

Bi. Katema amekuwa akilima mihogo kwa zaidi ya miaka 13. Amekumbana na changamoto nyingi lakini kwa sasa changamoto kubwa ni kupata mtaji.
Angependa kupata mkopo ili kununua pembejeo kama mbolea, viuatilifu na usafiri wa kusafirisha mihogo yake kutoka shambani kupeleka sokoni.

Anaelezea: “Tatizo ni kwamba hatupati mikopo. Mkopo kutoka benko unachukua muda mrefu mpaka kuupata, na ukipata mkopo utalazimika kulipa kila mwezi. Mihogo inachukua miezi sita mpaka saba [mpaka kukomaa] kuvunwa. Sasa nitapata wapi pesa ya kulipa benki kila mwezi?” Bi. Katema anapendelea kulipa mkopo wake baada ya kipindi cha mwaka mmoja, pindi anapokuwa amemaliza kuvuna na kuuza mihogo yake.

Wanawake wengi wanataabika kukuza uzalishaji kwasababu wanashindwa kupata ardhi na mikopo. Kwa kitamaduni ardhi anarithishwa mtoto wa kiume. Na kwa familia zilizo nyingi, ni mwanaume ndiye anamammuzi ya matumizi ya pesa.

Bi. Katema anandoto za kununua ardhi zaidi na kununua trekta. Lakini hawezi kuongeza shamba lake la mihogo bila kupata mikopo. Mbali na vikwazo hivi bado anauzwezo wa kuzalisha na kutunza familia yake.

Bi. Katema ni mjane anaye walea wajukuu wake watatu. Kipato anachopata kwa kupanda mihogo inamsaidia kulipa ada za wajukuu wake.

Mwanaidi Shabani Muhama anapanda mihogo katika kijiji hiki pia. Mkulima huyu wa miaka 46 anakubali kuwa mikopo ya muda mfupi haimnufaishi mkulima kama yeye.

Bi. Muhama anasema, “Tuna matatizo na mikopo…. Wanahitaji kutambua sisi ni wakulima. Inachukua miezi sita kuvuna mihogo. Tunahitaji angalau mkopo wa mwaka mzima.”

Hamza Suleiman ni afisa ugani wa Bagamoyo, na anafanya kazi katika wilaya inayojumuisha Kongo. Ana washauri wakulima kuenda katika mashirika madogoadogo kupata mikopo. Kwa mfano, benki za kijamii zina riba ndogo na masharti nafuu.

Bw. Suleiman anaongeza kwa kusema: “Tunawashauri wakulima kuchukua mikopo kwa wasambaza pembejeo [wauza vifaa vya kilimo] ili angalau wapate masharti nafuu ya vifaa vya kilimo kama trekta. Ni vigumu kwa mkulima mmoja kupata trekta, lakini wakiwa wakulima au kikundi kikaomba trekta, wanaweza kupata, na wanaweza kuwasaidia wakulima wengine pia.”

Bi. Katema na Bi. Muhama wanafikiria kujiunga na wanachama wengine kijijini ili kununua trekta.

Bi. Muhama anawahimiza wakulima wenzake kufuata ushauri wa afisa ugani na kutumia vifaa vya kilimo ili kuongeza uzalishaji. Anasema kuwa, kama benki inatoa mikopo kwa masharti nafuu, wanawake wakulima wengi wataweza kuboresha kilimo na kuongeza uzalishaji, na kuhudumia familia zao vizuri.

Simulizi hii imeandaliwa kwa msaada wa USAID’s New Alliance ICT Extension Challenge Fund, kupitia mfuko wa kimataifa kwa maendeleo ya kilimo Tanzania. Kwa taarifa zaidi kuhusu mfuko huu, tafadhali tembelea: https://www.ifad.org/ [1]