- Barza Wire - https://wire.farmradio.fm -

Tanzania: Wanawake hutumia viatilifu kuthibiti wadudu na magonjwa kwenye maharage

Ni msimu wa kupanda mazao wilayani kasulu, na Bibi Ziporah Mussa yupo katika shamba lake anapanda maharage. Hali ya hewa ni tulivu na jua linachomoza kwa umbali. Bibi Ziporah anasema “Nimekua nalima mazao takribani miaka 15 sasa … ya aina mbali mbali za maharage, ninapanda Lyamungo na soya ya njano kwa kiwango kikubwa.”

Bibi Ziporah anaishi katika kijiji cha Nyumbigwa, wilayani kasulu mkoa wa Kigoma magharibi mwa Tanzania. Anasema “wadudu wanaojulikana kama butotos kwa lugha ya Kiha wamekua wakiathiri maharage kwa misimu miwili iliopita. Wadudu hawa wana athiri aina zote za maharage.”
Anasema kwamba viatilifu vinapatikana kijijini mwao, na Kasulu mjini takribani kilomita 10. Lakini ni ghali sana na mara zote amekua hanunui.

Mara nyingine anapendelea kutumia madawa ya asili au kienyeji. Anasema kwamba majani ya mti unaoitwa ntibuhunwa (Tephrosia vogelii) kwa lugha ya kwao inatumika kutibu butotos. Anaeleza “Anasaga majani na kuchanganya na pilipili na kuloweka kwenye maji kwa masaa 24.” Anaongezea kwa kusema “Pia nina kata na kusaga matunda ya mti unaoitwa vitembwatembwa, na kuweka kwenye maji kwa masaa 24.”

Baada ya masaa 24 Bibi Ziporah anachuja kimiminika na kutumia kama kiatilifu kuulia wadudu. Anaeleza “Ninaweka kimiminika katika ujazo wa lita 10 katika plastiki na kutumia ufagio laini ama majani ya mti, majani laini kunyunyuzia dawa katika maharage.”

Esther Mpuzu pia analima maharage katika kijiji cha Nyumbigwa. Anasema wadudu wameathiri karibu aina zote za maharage katika shamaba lake, lakini aina ya maharage ya Lyamungo inastahimihi wadudu na magonjwa. Lakini, tahadhari, kama hutopanda kwa muda aina hii pia inaweza kuathirika.

Anasema “Kalabhutahe imekua na matokeo makubwa kwenye mahindi na pia nimeona hayo kwenye maharage pia lakini butotos ni moja ya gonjwa ambalo limeathiri maharage kwa kiasi kikubwa”.

Bibi Mpuzu anasema kwamba tatizo la magonjwa lilianza misimu miwili iliyopita. Kabla ya hapo, maharage yalikua hayaathiriwi na wadudu na magonjwa katika eneo lake. Anasema, “Sikuweka nguvu kubwa kutatua tatizo kwa sababu ilikua imeathiri sehemu ndogo tuu ya shamba langu.”
Katika kuthibiti wadudu, anasema, “Nimejaribu kutumia viatilifu nilivyozoea kutumia kwenye mahindi. Viatilifu hivyo havikufanya kazi kwani wadudu waliendelea kushambulia maharage.”

Michael J. Sabibi ni afisa ugani katika eneo hilo. Anasema “Ninatembelea wakulima mara kwa mara kubaini aina ya wadudu na magonjwa yanayoathiri mazao. Ninawashauri namna ya kutatua tatizo hilo.”

Bw. Sabibi anasaidia wakulima kuelewa namna sahihi ya kutumia viatilifu na kwa wakati sahihi. Anaeleza “Pia ninawashauri kutumia kilimo mzunguko na kung’oa maharage yaliyokwisha athirika ili kuzuia kusambaa na kuathiri maharage mengine.”

Anasema kuna wadudu na magonjwa mengi lakini butotos na Mnyauko Fusarii (Fusarium wilt) ndio huathiri maharage kwa wingi. Anaongezea kwamba “Wakulima wengi hawawezi kununua viatilifu kwa sababu ni gharama kubwa.”

Lakini kulingana na J.J Rubuye, Mshauri wa mambo ya kilimo wa mkoa wa Kigoma, mojawapo ya sababu zinazowafanya wakulima waseme hawawezi kununua viatilifu ni kwamba wanathamini sana kununua viatilifu mwanzoni mwa msimu wakati wana pesa kidogo. Kama wakulima watanunua viatilfu mapema – baada ya kuuza mazao – Bw. Rubuye anasema kwamba viatilifu vinapatikana kwa bei nzuri, na wakulima wataweza kuthibiti wadudu na magonjwa.

Pia Bw. Sabibi anasema kwamba wakulima wanatumia majani ya mti ntibuhunwa (Tephrosia vogelii). Wanasaga majani na kuloweka kwa masaa kadhaa alafu wanachuja kimiminika na kunyunyuzia kwenye maharage yao. Anaongeza kua haijawa wazi kipimo gani ni sahihi cha kutumia; wakulima wanatumia tuu wakati kuna tatizo kwenye maharage.

Amesema “Inaonekana kua madawa ya kienyeji yanafanya kazi kwa sababu wakulima wengi wanatumia.”

Bibi Ziporah anakubali kua madawa ya kienyeji yanaonekana kufanya kazi vizuri ingawaje ni rahisi sana kuondolewa na mvua inaponyesha, kipindi ambacho madawa hayo huingia kwenye vyanzo vya maji vya sehemu hiyo. Kama ilivyo kwa viatilifu, dawa za kienyeji zinaweza kua na athari mbaya kwa samaki na wanyama wengine wa majini.

Taarifa hizi zimeletwa kwenu kwa msaada wa AGRA, Muungano wa Mapinduzi ya Kijani Afrika kupita mradi shirikishi wa “Kuongeza kipato na uhakika wa chakula kwa wakulima Magharibi mwa Tanzania/Karagwe”. Hata hivyo, sio lazima kua maoni yaliyowasilishwa kwenye kijarida hiki ni maoni ya AGRA au shirika linguine lolote.