- Barza Wire - https://wire.farmradio.fm -

Tanzania: Wanakijiji wakisafiri mbali maporini kutafuta mboga za asili zinazozidi kupotea kutokana na shughuliza kibinadamu

Lazack Kesongo anazama katika maji ya kina kifupi cha mto Mara, polepole akivuka ng’ambo kwenda kutafuta mboga ya kirerema. Kirerema ni mboga za majani za asili zenye rangi ya kijani, zenye kamba ambazo hujisokotea kwenye miti na kupanda juu kwenye matawi ya miti mikubwa iitwayo macheno, miti hii huota sana sana kando kando ya mito. Mto Mara ni moja kati ya mito mikubwa nchini Tanzania inayomwaga maji yake katika ziwa Vicktoria.

Miaka ya 1980 wakulima kama Bw Kesongo hawakulazimika kuvuka mito kwenda kutafuta mboga. Mkoani Mara uoto juu ya ardhi ulikuwa wa kuvutia na watu walikuwa wakichuma mboga za asili kama hizi na uyoga katika maeneo ya wazi na mashambani mwao. Lakini leo hii watu wanalazimika kusafir umbali hadi wa kilometa 20 kutafuta mboga hizi za asili kwaajili ya lishe na matibabu.

Bw. Kesongo amekuwa akilima katika kijiji cha Matongo kwa zaidi ya miaka 30 wilayani Tarime kando kando mwa mto Mara. Anasema kwa ujumla mboga za asili ni dawa. Kwa mfano majani ya rikororobhe ni mmea wenye majani madogo.

Bw. Kesongo anaelezea: “Rikororobhe inaimarisha mfumo wa mzunguko wa damu mwilini, [na majani mengine ya asili yanasaidia kutibu] maumivu ya tumbo baada ya kujifungua.” Majani haya ni muhandighonkore, rityambwi, limenyo, mgagani, na mlenda.

Defroza Hamis anaishi katika kitongoji cha Kegonga B, mkoani Mara. Anatumia aina mbalimbali za mboga za majani kutibu magonjwa. Kwa mfano alipata maumivu ya tumba baada ya kujifungau, hivyo alichemsha kirerema na kunywa maji yake na ilimtibu maumivi ya tumbo.

Bi. Hamis anasema, “Hapo zamani, baada ya kutoka shuleni, wazazi walikuwa wakituambia tukachume mbga au uyoga kwaajili ya kupika lakini sasa uyoga haupatikani tena.” Anasema mazao haya yamekuwa hadimu baada ya watu kuongezeka, watu wamejenga nyumba na kusafisha mashamba ili kupanda mazao.

Nyabasamba Nyaiboha anauza maboga katika kitongoji Kegonga B. Anasema, zamani watu walikuwa wanapata mboga hizi kwa urahisi na wanazichuma bure. Lakini sasa, watu wanalazimika kuzinunua au kusafiri kwa umbali wa kilometa 10 kuzitafuta maporini.

Bi Nyaiboha anaelezea: “Kwa [sasa] tunalazimika kutembea umbali mrefu sana kupata mboga hizi. Tunauza fungu moja kwa shilingi 200 [sawa na Dola 0.09]. Ukiwa na familia kubwa utanunua mboga mpaka za shilingi 1000 [sawa na Dola 0.44]. Zamani tungeweza kupata mboga hizi bure vijijini. Lakini sasa kama huba hela ya kununua mboga, watoto wanaenda kulala na njaa.”

Baadhi ya sababu mbalimbali zinatajwa kupotea kwa mboga hizi. Baadhi ya watu wanakata mboga hizi na hawafanyi jitihada zozote za kuzipanda upya. Mifugo pia inakula na inakanyaga mboga hizi kupelekea jupotea.

Njonga William ni mtaalamu wa misitu Halmashauri ya wilaya ya Tarime. Anasema mboga za asili zimepotea kutoka na shuguli za binadamu zinaharibu mazingira na madadiliko ya tabia ya nchi.

Bw. William anaongeza: “Kuwepo na sheria kuwa, mtu anapokata mti, lazima waonyeshe kwanza kwamba waliotesha mti mwingine kabla ya kukata mti. Kwa wafugaji wanaotaka kufuga, wataalamu wanapaswa kuwashauri maeneo yanaoyafaa kufugia wanayama. Vitengo mablimabli lazima vishirikiane kutatua tatizo hili.”

Doto Mungo ni mtaalamu wa mazingira Halmashauri ya wilaya ya Tarime. Anasema, mbolea za viwandani zimechangia tatizo hili kwa kudhoofisha rutuba ya ardhi. Anasema pia kuwa mimea ya kisasa kama miti ya mikaratusi inafyonza maji mengi ardhini ambapo inapelekea na kusababisha kudhoofika kwa mmea na mboga za asili.

John Marwa anamaelezo mengine. Bw. Marwa ni katibu tawala wa wilaya ya Tarime. Anasema, mboga za majani zinapotea kwasababu zimezidiwa na aina tofauti za aina za mboga kama Kabichi. Vijana wanachukia kula mboga za asili ambazo wazazi wao walikuwa wakila.

Akishikilia juu tawi la mmea za mboga za majani aina ya kirerema, Lazack Kesongo anasema, yeye na wakazi wengine wanataka kujua namna watakavyo washwishi watu kulima mboga hizi za asili. Anasema, “Watu wafundishwe jinsi ya kutunza mazingira ili kuokoa mboga hizi za asili, kwasababu zina afya sana na zinagharama nafuu kulinganisha na hizi mboga nyinginezo.”

Uniterra wamefadhili simulizi hii. Shirika la Uniterra Tanzania linafanyakazi na wadau wa ndani ya nchi katika secta ya matunda, mbogamboga na utalii kuwasaidia vijana wadogo na wanawake kupata nafasi nzuri katika nyanja za kiuchumi. Uniterra inapokea msaada wa kifedha kutoka serikali ya Canada, kupitia Global Affairs Canada, www.international.gc.ca [1]. Jua zaidi kuhusu Uniterra Tanzania katika Facebook katika tovuti hii: facebook.com/wusctanzania [2]