- Barza Wire - https://wire.farmradio.fm -

Tanzania: Magonjwa na ukosefu wa malisho unazuia upatikanaji wa masoko ya nje ya mifugo

Ni majira ya saa nne na nusu asubuhi, anga limeng’aa na hali ya hewa ni shwari. Chui Meja anaangalia ngombe, kondoo na mbuzi zake kwa makini akiwa anawatoa kutoka zizini kwenda malishoni. Akiwa na miaka 39 amevalia suruali ya rangi ya udongo na shuka jekundu la kimila la jamii ya kimaasai.

Bw. Meja anasema kwamba hawezi kusafirisha mifugo yake na bidhaa za wanyama kwa sababu ya changamoto inayohusiana na magonjwa na malisho yasiyo ya kuridhisha.

Anaelezea “Wanyama wengi wamekonda kwa sababu ya kutembea umbali mrefu wakifuata chakula na maji. Naweza kuhesabu hata mbavu zao, na wengi wao hata hawana vigezo vya kuchinjwa. Wengine wameathirika na magonjwa kama Homa ya Pwani ya Mashariki. Ni ngumu kuwauza wanyama hao (kwenye masoko ya nje).”

Bw. Meja kwa sasa anaishi kijiji cha Kitonga, kilomita 90 kutoka Dar Es Salaam, kitovu cha biashara Tanzania.

Kupambana na hizi changamoto, amekua akitanga tanga na familia yake kwa miongo minne sasa sehemu mbali mbali Tanzania akitafuta maji, malisho na maeneo ambayo hayana magonjwa.

Anasema kwamba familia yake inateseka wanavokua wanahama hama kwa sababu ya kutokua na kushindwa kuuza mifugo katika masoko ya nje. Kwa sababu ya uhaba wa malisho, Mifugo ya Bw. Meja ni dhaifu na wanaonekana wamezeeka. Masoko ya nje yanahitaji mifugo yenye ubora wa hali ya juu na bidhaa zitokanazo na mifugo hio.

Engelbert Bilashoka ni meneja wa kanda ya kati katika Mamlaka ya Chakula na Dawa. Anakubaliana na Bw. Meja kwamba hawawezi kusafirisha ama kuuuza mifugo yao katika masoko ya nje kwa sababu ya magonjwa pamoja na malisho hafifu. Licha ya kwamba Tanzania ni nchi ya tatu Africa kwa uzalishaji wa mifugo.

Bw. Bilashoka anaeleza “Wafugaji wengi haswa wale wanaohama hama ambao Tanzania, hawana maeneo ya malisho ya kutosha. Pia hawana mipango/programu zinazowawezesha kulisha mifugo yao.

Aliongeza “Mifugo hutegemea malisho bila ya kua na nyongeza ya aina nyingine yoyote ya virutbisho. Hii ndio sababu inayopelekea kuchelewa kufikia uzito unaostahili kwa kuchinjwa. Hii imepelekea kutofikia uzalishaji wa nyama unatakiwa na masoko ya nje.”

Wafugaji wanao hama hama huuza mifugo yao katika minada kwa wanunuzi kutoka kwenye makundi ya wasindikizaji wa nyama, au wanunuzi kutoa Comoros, Kenya, DRC, na hata Falme za kiarabu.

Nicholai Chiweka ni Afisa masoko na utafiti kutoka Bodi ya nyama Tanzania. Anasema ugumu wa kuuza mifugo na bidhaa zitokanazo na mifugo katika masoko ya nje ni kutokana na ukosefu wa programu za malisho. Kwa sababu ya ufugaji wa kuhama hama, mifugo mingi inakosa uzito wa kutosha kuuza katika masoko ya nje. Kukidhi vigezo vya kuuza mifugo katika masoko ya nje ya nchi, wafugaji wanahitajika wapate mafunzo ya uhakika ya namna ya kuwalisha mifugo kabla ya uchinjaji.

Tanzania, maeneo mengi ya wazi ambayo yalipaswa kua ni sehemu ya malisho, yamefungwa na kufanywa kua hifadhi za taifa kama vile Manyara, Serengeti, Loliondo na Ngorongoro. Ili kuhifadhi wanyama pori, serikali imebadilisha matumizi ya maeneo hayo kutoka malisho ya mifugo na kua hifadhi za wanyama pori. Kuna matumaini kwamba serikali itaona umuhimu wa kupanga na kutenga maeneo mengine ya malisho ili kufidia yale maeneo ya malisho yaliyochukuliwa kwaajili ya uhifadhi.

Faustine Lekule ni profesa katika Chuo kikuu cha kilimo cha Sokoine Tanzania. Anasema kwamba ili wakulima kama Bw. Meja waweze kunufaika kiuchumi na ufugaji kuna umuhimu wa kutenga maeneo ambayo hayana magonjwa, kuimarisha sehemu za machinjio, na kuanza kusindika bidhaa zitokanazo na mifugo.

Bw. Lekule anaeleza “Japokuwa hatuwezi kumaliza tatizo la magonjwa nchini ni muhimu kutenga sehemu maalumu ama kisiwa ambapo kutakuwepo na uangalizi wa hali ya juu katika kuhakikisha maeneo hayo hayatashambuliwa na magonjwa.”

Aliongezea “Tanzania imeimarisha viwango vya machinjio ambavyo vitathibitishwa na bodi ya kimataifa na kuruhusu kusafirisha nyama nje ya nchi. Badala ya kufikiri kuuza nyama pekee inapaswa kufikiri namna ya kuelekeza nguvu katika usindikaji…Kuna masoko makubwa nchini China na mashariki ya kati ya bidhaa za nyama au mifugo.”

Bw. Meja anasema ataendelea kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine kutafuta malisho ambayo hayana magonjwa. Anaeleza “Tumetumia muda wote wa maisha yetu kuhama na mifugo yetu. Sio kwa kupenda kwetu lakini ni lazima kufanya hivyo. Tutaendelea kutafuta maeneo ambayo hayana magonjwa kwa mifugo yetu.”

Taarifa hizi zimepatikana kwa kuwezeshwa na Elanco Animal Health.