- Barza Wire - https://wire.farmradio.fm -

Nigeria: COVID-19 huathiri mapato ya wafanyakazi wa mashambani

Ni mapema asubuhi siku ya Jumapili, joto ni karibu nyuzi joto 25, na msimu wa mvua ndio kwanza umeanza. Akiwa na uso wa huzuni, Murtala Abbas mwenye umri wa miaka 40 anafunga redio ndogo na fimbo ya kupuria mchele kwenye baiskeli yake na kuendesha polepole huku akisikiliza redio. Bwana Abbas anasafiri kwenda kufanya kazi katika shamba la mpunga karibu kilomita 10 kutoka nyumbani kwake.

Anasema: “Nilikuwa nikisisimka sana mwanzoni mwa kila msimu wa mvua kwa sababu nilikuwa nikipata kazi zaidi ya kufanya mashambani na nilikuwa nikipata pesa zaidi kusaidia familia yangu. Lakini mwaka huu, hali ni tofauti kwa sababu COVID-19 imeathiri vibaya kazi yangu na mapato yangu.”

Bwana Abbas ni mfanyakazi wa shamba anayeishi katika kata ya Bari katika eneo la serikali ya mtaa wa Rogo katika Jimbo la Kano la Nigeria. Ana wake watatu na watoto 13 na amekuwa akifanya kazi kwenye mashamba ya mpunga kwa karibu miaka 20.

Anasema serikali ilihitaji watu kukaa nyumbani siku tano kwa wiki kati ya katikati ya Aprili na katikati ya Julai. Hii ilimaanisha kwamba Bwana Abbas na wafanyikazi wengine wa shamba wangeweza kufanya kazi siku mbili tu kwa wiki kwenye mashamba ya mpunga.

Anasema kipato chake kilipungua sana na alikuwa hajawahi kukabiliwa na hali ngumu kama hiyo. Bwana Abbas anaelezea, “Kabla ya COVID-19, kipato changu kwa siku kilikuwa naira 900 za Nigeria ($ 2.32 US), lakini wakati kufungiwa kulipoanza, nilikuwa nikipata naira 400 za Nigeria ($ 1.03 US) kwa siku.” Kiwango chake cha kila siku kilipungua kwasababu shida ilizuia idadi ya masaa ambayo angeweza kufanya kazi shambani hata siku zake za kazi.

Familia yake ililazimika kuwa na milo miwili tu kwa siku. Anaongeza, “Bei ya chakula pia iliongezeka kutokana na janga la COVID-19 na hakukuwa na msaada wowote kutoka kwa serikali kwetu sisi wafanyakazi wa shamba.”

Sagiru Rogo ni mfanyakazi wa shamba kutoka kijiji cha Liman katika Jimbo la Kano. Anasema kupunguzwa kwa kazi kwenye shamba kwasababu ya kufungiwa ndani iliathiri sana familia yake na hakuweza kununua chakula.

Bwana Rogo anaelezea: “Pamoja na watoto wangu kumi, mara chache sana nilikuwa naweza kumudu milo mitatu kwa ajili ya familia yangu kwasababu ya kipato kidogo kama matokeo ya COVID-19. Nilikuwa na baiskeli, ambayo nilikuwa nikitumia kwenda kufanya kazi kwenye mashamba, lakini ilibidi niiuze ili kugharamia matumizi ya kila siku kutokana na kipato kidogo nilichokipata.”

Anaongeza, “Mambo yalikuwa magumu sana kwa sababu pia nililazimika kuahirisha harusi ya binti yangu kwasababu ya janga hili na kuzuiliwa kutotoka nnje.”

Jumalo Ado ni mfanyakazi mwingine ambaye anafanya kazi kwenye mashamba katika Jimbo la Kano. Anasema hakuamini kuhusu COVID-19 hapo mwanzoni, lakini mawazo yake yalibadilika baada ya kusikiliza redio. Sasa anafuata hatua za tahadhari kama vile kunawa mikono na sabuni, kuzingatia suala la kukaa umbali fulani kutoka kwa watu wengine, na kutumia barakoa kila anapoenda kazini.

Bi Ado anasema kwamba mashamba ambayo anafanya kazi yalikabiliwa na changamoto za kifedha kwa sababu ya COVID-19 na kwasababu hii, wafanyikazi walipokea chakula badala ya pesa.

Bwana Abbas anasema ni ahueni kubwa kwamba kipindi cha kufungiwa kimeisha. Anasema atafanya kazi kwa bidii kupata pesa zaidi ili kusaidia familia yake, lakini bado anaogopa. Anaelezea: “Ingawa ninajitahidi sana kupata pesa zaidi kama mfanyakazi, ninaogopa kwa sababu gharama ya maisha imeongezeka kwa sababu ya COVID-19 na bado nina uzoefu ikiwa kile nitakachotengeneza kitatosha kununua chakula na vitu vingine.”

Ili kukabiliana na athari za COVID-19 na kujiandaa kwa uwezekano wa kufungiwa tena siku zijazo, Bwana Abbas anasema ataanzisha biashara ambazo zinaweza kumsaidia kupata kipato wakati wa nyakati ngumu.

Anaelezea, “Kama mpango wa dharura wa matukio ya siku za usoni ya kufungiwa, mbali na kufanya kazi katika mashamba, nitaanzisha biashara ndogo kama kuuza kuni na makaa ya mawe.”

Rasilimali hii imeandaliwa kwa msaada wa kifedha kutoka kwa serikali ya Canada uliotolewa kupitia Global Affairs Canada.

Picha: Wakulima kaskazini mwa Ghana wakielekea shambani, 2015. Imechukuliwa na: Jesse Winter / Farm Radio International