- Barza Wire - https://wire.farmradio.fm -

Kenya: Miti husaidia wakulima katika urutubishaji wa ardhi na kuongeza uzalishaji wa mazao

Beatrice Wamalwa anatabasamu huku akiwa anatembea katika shamba lake, akiwa amezungukwa na miti. Anaangalia kwa mshangao idadi ya miti na kukumbuka wazi jinsi ambavyo shamba hilo lilivyokua likionekana mwaka 2009.

Bibi Wamalwa anasema kwamba, kwa sababu hakupanda miti katika shamba lake mvua ilinyesha na kusomba udongo wote. Shamba lake likawa halina rutuba na uzalishaji katika shamba lake la heka moja ukapungua.

Ili kubadilisha hali hiyo, alianza kufanya kilimo mseto mbinu ambayo wakulima hupanda miti ama vichaka kuzunguka mazao yao. Anaelezea “Nilichimba mitaro kuzunguka shamba langu na kupanda miti inayokua kwa haraka zaidi inayojulikana kwa jina la Grevillea robusta na miti mingine ya kienyeji. Leo, hata kama mvua kubwa ikinyesha udongo wangu hauwezi kuchukuliwa kwa sababu imeifadhika vizuri.”

Bibi Wamalwa ni mama wa watoto sita na bibi anaeishi kijiji cha Tembelela magharibi mwa Kenya kaunti ya Bungoma. Amejifunza upandaji miti huhifadhi ardhi na kuimarisha udongo kutoka kwa Vi-Agroforestry, shirika lisilo la kiserikali lililowafundisha wanachama 51 kutoka katika kikundi chake miaka kumi iliyopita.

Anasema “walitufundisha kwamba ukataji miti husababisha mashamba yetu kuchomwa na jua na matokeo yake yanakua yana uzalishaji hafifu.”

Bibi Wamalwa amepanda maharage, mboga za kienyeji, pilipili (capsicum), mahindi, na viazi vitamu. Alianza kupanda miti ya aina ya Grevillea robusta mwaka 2009 katika mzunguko wa shamba lake na katika sehemu maalumu katikati mwa shamba lake. Miti ilibaki shambani kwa muda mrefu lakini haishindanii virutubisho vilivyopo ardhini na mazao yake kwa sababu mizizi ya miti ilikua imezama chini sana. Anasema miti ilimsaidia sana katika kutunza udongo wake na kupunguza mmomonyoko wa ardhi. Mbao zitokanazo na miti hio hutumika katika kujenga samani, na necta yake huvutia nyuki.

Miti inapoangusha majani yak echini, majani hayo humpatia Bibi Wamalwa na takribani sentimita 30 hadi 40 za matandazo, ambayo husaidia katika kuhifadhi unyevu na ardhi. Matandazo hayo yanapooza, husaidia kuongeza rutuba ardhini.

Albert Luvanda ni Mtafiti kutoka katika Taasisi ya misitu Kenya. Anasema wakulima wanapaswa kupunguza matawi ya miti ya Grevillea robusta kama itaanza kukinzana ama kushindania chakula na mazao ama kushindania jua.

Ezekiel Odeo ni mkulima katika eneo hilo ambae alianza kupanda miti aina ya Grevillea robusta katika shamba lake baada ya kupata mafunzo kupitia shirika la Vi-Agroforestry. Anasema kwamba, mbinu za kilimo msemo zimemkomboa kutoka katika umaskini.

Kuepuka wanyama kula ama kuharibu miti ya Grevillea robusta baada ya kuvuna, Bw. Odeo alipunguza majani ya miti na kulisha mbuzi na ngombe wake na kutumia mashina kama kuni.

Amos Wekesa ni mshauri wa mambo ya hali ya hewa kutoka shirika la Vi-agroforesrty. Anasema kwamba wakulima wanaofanya kilimo mseto katika maeneo yao wameweza kuongeza uzalishaji wa chakula na kipato. Bw. Wekesa aliongeza “wanaweza kuhudumia familia zao vizuri zaidi na wameweza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.”

Bw. Odeo anasema anapata zaidi ya dola za kimarekani 2,500 kutokana na mbinu za kilimo mseto. Hii imemsaidia kuwapeleka watoto shule pamoja na kujengea familia yake vyumba viwili vya kulala kwa kutumia matofali. Anasema “Zaidi ya asilimia 70 ya kipato ninachokipata leo kinatokana na kilimo.”

Mwaka huu, Bibi Wamwalwa alivuna magunia 60 yenye uzito wa kilogram 90 kutoka katika kila shamba la ekari moja, pamoja na magunia mawili ya maharage. Kabla hajapanda miti ya Grevillea robusta alikua akivuna magunia matatu ya kilogramu 90 ya mahindi na kilogramu 40 ya maharage.

Anasema “Ni miujiza kwamba miti yangu inaninufaisha na kunipa fedha za ziada.”