- Barza Wire - https://wire.farmradio.fm -

Ghana: Athari za kiuchumi za COVID-19 husababisha unyanyasaji wa kingono na kijinsia

Ni saa nne alasiri na Abena Nhiyra wa miaka 17, ambaye ni mjamzito, amerudi kutoka shuleni. Anaonekana amechoka na analia wakati anajaribu kuelezea ni vipi alipata ujauzito wakati ambapo shule ilifungwa kwasababu ya COVID-19.

Bi Nhiyra ni mjamzito kwasababu alinyanyaswa kingono na kijana katika jamii yake ambaye alitumia fursa za changamoto za kifedha za mama yake-ambazo ziliongezeka kutokana na COVID-19. Mama yake huuza mboga sokoni. Lakini ili kudhibiti kuenea kwa COVID-19, serikali ilifunga soko kwa karibu miezi miwili.

Bi Nhiyra anaelezea: “Hakukuwa na kitu cha kupika siku hiyo. Mama yangu aliniambia nimfuate nyumbani kwake kupata kifuko cha mchele. Mara tu nilipoingia nyumbani kwake, alianza kunibusu na kuniambia kuwa nikifanya mapenzi naye, atashughulikia familia yetu. Nilisema hapana, lakini alinilazimisha na kunionya nisijulishe mtu yeyote.”

Bi Nhiyra anaishi na mama yake na ndugu zake watatu huko Kintampo, katika mkoa wa Bono Mashariki mwa Ghana. Yuko mwaka wa tatu wa shule ya upili ya junior na anajiandaa kufanya mtihani wake wa cheti cha elimu ya msingi mwaka huu. Ingawa yeye ni mjamzito, anasoma shule ili aweze kufanya mitihani yake ya mwisho.

Ghana ilirekodi kisa chake cha kwanza cha COVID-19 mnamo mwezi Machi. Wakati wengine wameshakufa kutokana na ugonjwa huo, wengine wengi wamefanywa kuwa hatarini zaidi, haswa wanawake na wasichana. Ukatili wa kijinsia umeongezeka wakati wa COVID-19, ikisababishwa na sababu kadhaa, pamoja na msongo wa mawazo utokanao na vizuizi na ukosefu wa ajira na mapato.

Mansah Dokua ni mwanamke asiye na mume na mwenye mtoto mmoja. Alikuwa mwalimu katika shule ya binafsi, lakini anasema ni ngumu sana kulipa kodi na kununua chakula kiasi kwamba alikaribia kushiriki uasherati ili kuishi.

Bi Dokua anaelezea: “Kwasababu ya janga la COVID-19, nilipoteza kazi. Ni ngumu kuishi. Mimi ni mwanamke na kwa sababu ya mafadhaiko, nilikuwa karibu kuanza kuhama kutoka kwa mwanamume mmoja kwenda kwa mwingine, lakini baada ya mawazo ya pili, niligundua kuwa haikufaa kufanya hivyo.”

Anaongeza: “Niliamua kumwomba baba wa mtoto wangu msaada. Lakini hakuwa tayari kuniunga mkono na kuchukua jukumu lake. Mazungumzo yetu yakawa ya kugombana na alinishambuliwa na kesi bado ipo kituo cha polisi. “

Kulingana na Bi Dokua, hangemuomba mtu huyo msaada, lakini alifanya hivyo kwasababu ya shida zilizoletwa na COVID-19.

Michael Tagoe ni Afisa wa Programu ya Vijana katika Jumuiya ya Planned Parenthood ya Ghana. Anasema kuwa janga la COVID-19 limeongeza kiwango cha unyanyasaji wa kingono na kijinsia, na pia aina zingine za unyanyasaji wa kijinsia, pamoja na ukeketaji wa wanawake, mimba za utotoni, utoaji mimba usio salama, na ndoa za utotoni.

Bwana Tagoe anasema, “Ukatili wa kijinsia umetokea kwasababu ya kufungwa kwa shule na hali ya vizuizi kwasababu ya COVID-19.”

Ingawa wasichana wanakabiliwa na changamoto nyingi na zenye wasiwasi katika kujaribu kuendelea na masomo yao baada ya ujauzito na kujifungua, Bi Nhiyra ameazimia kumaliza shule. Anaelezea: “Nimeapa kuendelea na masomo baada ya kujifungua mtoto wangu. Hii ni bila kujali changamoto na unyanyapaa ninaoweza kukabiliwa nao kama mama mwenye umri mdogo. Nitafanya hivyo ili niweze kufikia malengo yangu hapo baadaye.”

Rasilimali hii imeandaliwa kwa msaada wa kifedha kutoka kwa serikali ya Canada uliotolewa kupitia Global Affairs Canada.