- Barza Wire - https://wire.farmradio.fm -

Burkina Faso: Amepona ugonjwa wa virusi vya Corona, mwandishi wa habari Issaka Lingani anasema alikuwa na bahati kuliko wengine

Katika miaka yake sitini, Issaka Lingani ni mwandishi wa habari na mkurugenzi wa chapisho la kila wiki la Maoni huko Ouagadougou. Anajulikana zaidi nchini Burkina Faso kwa nafasi zake za kisiasa, ambazo anashiriki wakati wa mijadala ya kwenye runinga. Anajulikana pia kwa kupima na kukutwa na maambukizi ya COVID-19.

Mnamo mwezi Aprili, Bwana Lingani alitangaza kwenye ukurasa wake wa Facebook kwa ucheshi kidogo. Anaamini alipata virusi hivyo wakati wa kusafiri kutoka Abidjan. Labda kwenye uwanja wa ndege. Labda kwenye ndege.

Mpaka Julai 15, kumekuwa na visa 1,037 vya maambukizi ya COVID-19 huko Burkina Faso na vifo 53. Angalau watu 880 walikuwa wamepona na 102 walikuwa wakitibiwa.

Bwana Lingani alishuku kwanza alikuwa anaumwa wakati anaugua homa, maumivu ya kichwa, kukosa usingizi, na hisia kubwa ya uchovu. Aliwaza kwanza juu ya malaria. Kisha homa ya dengue. Lakini vipimo hivyo vyote vilionyesha hana.

Baada ya hapo aliamua kuwasiliana na timu inayohusika na COVID-19 ili kupata uhakika. Anaelezea: “Katika simu yangu ya kwanza, waliniambia kuwa sina COVID-19. Lakini kwa sababu nilikuwa bado mgonjwa, niliwapigia tena kusisitiza. Niliwauliza watu wengine, pamoja na daktari wangu wa huduma za msingi, kuwaita pia.”

Baada ya siku tatu, timu ya matibabu ilifika nyumbani kwa Bwana Lingani. Anakumbuka, “Walikuja na timu yenye kuvutia. Walijitakasa kwanza kabla ya kuvaa nguo zao za kujifunika ili kuchukua sampuli ya kwenye pua.”

Baada ya kusubiri kwa siku mbili, Bwana Lingani alijulishwa kwa njia ya simu kwamba kipimo chake kimeonyesha ana maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Corona. Anasema, “Siku hiyo hiyo, timu nyingine ilifika, wakati huu wakiwa na gari la kubeba wagonjwa, kunichukua na kunipeleka hospitalini, kingo’ra kikilia kitu ambacho kilivuta hisia za majirani zangu wote.”

Alipewa chakula karibu saa 6 jioni wakati akisubiri dozi yake ya kwanza ya dawa hospitalini. Anasema aliikataa na kudai atibiwe kwanza.

Alipokea dozi yake ya kwanza ya chloroquine na azithromycin karibu saa 10 usiku.

Ziara yake ya hospitali ilidumu kwa siku 10: Siku tano katika hospitali ya Tengandogo na siku tano katika Kliniki ya Princess Sarah, vituo viwili vya Ouagadougou ambavyo vinatibu wagonjwa wa COVID-19. Analalamika kuhusu hali ilivyo katika hospitali katika upatikanaji wa vifaa vya hospitalini na vitendea kazi. Anabainisha kuwa hatua za msingi za kupunguza kasi ya kuenea kwa COVID-19, kama vile kunawa mikono, haziwezi kuzingatiwa hospitalini kwa sababu ya ukosefu wa sabuni na jeli inayotokana na pombe, na akatumia fursa hiyo kumjulisha Waziri wa Afya wakati Waziri alipotembelea wagonjwa.

Lakini timu za matibabu katika hospitali zote mbili zilimvutia Bwana Lingani kwa kujitolea kwao katika kuwahudumia wagonjwa.

Bwana Lingani anakiri kuwa alikuwa na bahati kubwa kuliko wagonjwa wengine wengi aliowaona wanaougua ugonjwa wa Corona hospitalini. Anasema kuwa, mbali na wagonjwa wawili au watatu ambao wanaweza kuwa walikuwa katika miaka yao ya sitini kama yeye, wengine wote walikuwa kweli vijana wenye hali mbaya kutokana na ugonjwa wa virusi vya Corona.

Sasa kwa kuwa amepona na kurudi kwenye utaratibu wake wa kawaida, Bwana Lingani anasema hakuna tofauti katika jinsi majirani zake au wenzake wanamtendea. Lakini anawajua wengine ambao wamepona na ambao wanakabiliwa na unyanyapaa: majirani hawajawatembelea tangu gari la wagonjwa ilipopita kutafuta wagonjwa.

Rasilimali hii imeandaliwa kwa msaada wa kifedha kutoka kwa serikali ya Canada uliotolewa kupitia Global Affairs Canada.