- Barza Wire - https://wire.farmradio.fm -

Benin: Vyama vya wanawake vinapigania kujumuisha wanawake katika kufanya maamuzi

Ni saa 7 asubuhi siku ya Jumamosi katikati ya mwezi wa Septemba. Asubuhi ambayo wingu la kijivu limejaza anga huko Cotonou, mji mkuu wa kiuchumi wa Benin. Lakini hali mbaya ya hewa haijawazuia wanachama vijana wa kike wa taasisi kadhaa zisizo za kiserikali (NGOs), pamoja na wanaharakati na watendaji wa kisiasa, kukusanyika katika makao makuu ya Réseau Ouest-Africain des Jeunes Femmes Leaders, mtandao wa viongozi wa wanawake vijana katika Afrika Magharibi.

Wanawake wako hapa kwa ajili ya kuwasilisha ripoti kuhusu mzozo wa uchaguzi nchini Benin. Mtandao wa viongozi wanawake vijana uliandaa mpango unaoitwa “mwezi wa kujenga amani” kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Amani, Septemba 21. Mariette Montcho ndiye rais wa mtandao huo. Anasema, “Vijana na wanawake ndio wahanga wa kweli wa hali za mizozo. Kwa hivyo ni muhimu kuwashirikisha na kuwaelimisha. ”

Huko Benin, wanawake wametengwa katika michakato ya kufanya maamuzi na mihimili, haswa wakati wa shida. Wanawake ni 50.7% ya idadi ya watu wa Benin, ambayo inakadiriwa kuwa watu milioni 12. Lakini kuna wanawake 78 tu kati ya maafisa 1,815 waliochaguliwa nchini. Kati ya hao, 31 wako katika mabaraza ya manispaa. Ni mawaziri watano tu kati ya 24 wa serikali ambao ni wanawake. Manaibu nane tu kati ya 83 ni wanawake.

Françoise Agbaholou ndiye mratibu wa kitaifa wa NGO inayoitwa Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (Women in Law and Development in Africa). Anaelezea: Uwakilishi duni wa wanawake na swali la kushiriki katika vyombo vya maamuzi ni matokeo ya vikwazo vya kijamii na kiuchumi, kiwango cha juu cha kutokujua kusoma na kuandika miongoni mwa wanawake, umaskini wa wanawake, ukosefu wa uwezeshaji wa wanawake, kutokuwa na nia ya kushiriki katika siasa, na shida ya hadhi ya wale wanaothubutu kuwa na nia ya kushiriki. ”

Kama sehemu ya juhudi zao za kuwashirikisha wanawake zaidi katika vyombo vya maamuzi, Benin ilipitisha sheria juu ya haki sawa mwaka 2019, lakini imepata shida katika kuitekeleza.

Bi Montcho anasema mtandao wake wa viongozi wa wanawake haukuhusika katika kiwango chochote cha mchakato wa kufanya uamuzi na hawakushirikishwa kuhusu hatua kama vile kukaa umbali kati ya mtu na mtu au kufungwa kwa soko. Vyama na mitandao mingine inalaumu kwamba pia hawakushirikishwa katika mchakato wa kufanya uamuzi.

Katika Afrika ya Magharibi, wanawake wako katika mstari wa mbele wa shida za kiafya kwasababu mara nyingi huwa na kazi mbaya katika sekta isiyo rasmi. Janga hilo limeongeza mazingira magumu kwa wanawake wanapopoteza mapato yao. Ukosefu wa chakula umeongezeka miongoni mwa wanawake na vile vile visa vya unyanyasaji wa kijinsia. Wanawake wengi wana ufikiaji mdogo wa habari juu ya shida za kiafya, na ufikiaji mdogo wa huduma msingi za kijamii kama vile afya na elimu. Sababu hizi zimeongeza zaidi kutokuwa na usawa kati ya wanaume na wanawake.

Kama njia ya kukabiliana na tatizo la COVID-19 nchini Benin, serikali ilichukua hatua kadhaa, ikiwa ni pamoja na uvaaji wa lazima wa barakoa katika maeneo ya umma na kufunga fukwe, maeneo ya ibada, na baa. Walianzisha pia “kamba za afya ya umma” zinazozunguka manispaa 10 zilizo hatarini kusini mwa Benin, na pia marufuku ya kutembea kwa magari ya uchukuzi wa umma.

Kuna mashirika mengi na mitandao ya wanawake ambayo yangeweza kushirikishwa kusaidia kukuza na kutekeleza hatua hizi. Bi Montcho anasema changamoto moja ni kwamba, “Mashirika ya kijamii hayafanyi kazi kwa harambee…. Kuna vyama vyenye mamlaka sawa, dhumuni sawa, malengo sawa, na ambayo hufanya kazi kwa kutengwa. Ni juu ya AZAKi kuchukua jukumu na kuwajibika.”

CARE ambayo ni shirika la kimataifa isiyo ya kiserikali, inafanya kazi nchini Benin na pia inajaribu kuwajumuisha wanawake katika michakato ya kufanya maamuzi. Aqueline Behanzin Dosseh ndiye mratibu wa programu katika shirika la CARE. Anasema, “Lazima tuhakikishe kuwa wanawake wanawakilishwa katika mifumo ya mashauriano katika ngazi za mitaa.”

Bi Dosseh anasema kuwa maafisa wanafahamu vikundi ambavyo viko katika maeneo yao. Anaongeza kuwa viongozi wa vikundi hivi vya wanawake wanahitaji kujumuishwa katika mifumo ya mashauriano katika ngazi za mitaa, manispaa, idara, na kitaifa. Anasema ni muhimu kuunda mchakato wa kuhamasisha na kuwasiliana, kupitia vyomba vya habari na kupitia watu ambao wana ushawishi mkubwa kwa wengine.

Vyama na mitandao ya wanawake wanapanga kuendelea kushawishi ili kuwaunganisha wanawake kwa ufanisi katika vyombo vya kufanya maamuzi nchini Benin.

Rasilimali hii imeandaliwa kwa msaada wa kifedha kutoka kwa serikali ya Canada uliotolewa kupitia Global Affairs Canada.

Picha: Kikundi cha akiba na mikopo cha kijiji cha wanawake nchini Benin.