- Barza Wire - https://wire.farmradio.fm -

Benin: Vikundi vya akiba na kukopa vijiji vinajitahidi kupambana kwa sababu ya COVID-19

Ni karibu saa 11 alfajiri ya Jumatano mwanzoni mwa Julai. Anga linaingia giza na mvua inaanza kunyesha. Véronique Ahissou anapanga meza, madawati, na viti kwenye duara chini ya makao ya muda nje ya nyumba yake. Anasema, “Leo sio siku ya soko, wanawake wa kikundi chetu wataweza kukutana. Tunatumai, mvua haitaongeza shida ya sisi kukutana kama ilivyo kwa virusi vya Corona.”

Bi Ahissou mwenye umri wa miaka 50 anaishi Dangbo, kijiji kilichopo kilometa 50 kutoka Cotonou, mji mkuu wa kiuchumi wa Benin. Yeye ndiye rais wa Gbénonkpô, kikundi cha kuweka na kukopa cha kijiji. Ni moja ya vikundi 2,000 vile ambavyo vinasaidiwa na Shirika Lisilo la Kiserikali la kimataifa, CARE.

Tangu shida ya ugonjwa wa virusi vya Corona ilipoanza, ni wanachama 10 tu kati ya 16 wa kikundi wameweza kukutana. Wanawake katika ushirika hawawezi tena kulipa hisa, au mchango wa kawaida, wa 200 FCFA ($ 0.36 US) na kikundi hicho hakiwapi wanachama tena mikopo. Wanawake pia wanajitahidi kuchangia 50 FCFA ($ 0.09 US) kama mchango wa mshikamano katika kikundi.

Vikundi hivi vya akiba na mikopo vijijini hufanya kazi kama usalama wa kijamii na kiuchumi. Wanawake huandaa hisa ambazo wanaweza kutoa mkopo. Wanatumia mikopo hiyo kufadhili biashara ndogo ndogo, pamoja na kununua mchele, tambi, mahindi, na bidhaa zingine ambazo huuza tena. Pamoja na mapato, wanaweza kuendelea kulipa hisa na pia kuendesha familia zao.

Mikopo ya kikundi hulipwa baada ya miezi mitatu kwa kiwango cha riba cha 5% kila mwezi. Riba husaidia kudumisha mchakato wa mkopo unaozunguka kwa faida ya wanachama wote. Na mfuko wa mshikamano unaruhusu kikundi kusaidia washiriki katika hali ngumu.

Lakini janga la virusi vya Corona limepunguza uwezo wa wanawake kujipatia kipato. Bibi Ahissou anaeleza: “Kwasababu ya COVID-19, biashara zetu hazitengenezi fedha kama ilivyokuwa hapo awali. Kwahiyo tumepunguza kiwango cha mkopo kutoka 15,000 FCFA ($27 US) mpaka 5,000 FCFA ($9). Kila mtu anachukua kiwango ambacho anaweza kurejesha. Kabla ya janga hili, jumla ya kiwango kikubwa cha mkopo ambacho mtu angeweza kuchukua ilikuwa ni 40,000 FCFA ($72 US).”

Fedha iliyokopwa huelekezwa katika biashara ndogo ndogo, lakini mdororo huo umewazuia wanawake kulipa mikopo yao. Wanasita kuchukua mikopo zaidi ingawa wanahitaji pesa kusaidia familia zao na kulipa hisa. Hii ni hali ya hatari.

Emilienne Hounton ni katibu mkuu wa kikundi kingine cha akiba na mikopo kinachoitwa Mignonmidé. Anasema, “Ijumaa iliyopita, wawakilishi kutoka Shirika lisilo la Kiserikali – CARE, walikuja kutuuliza maswali. Tuliwaambia kwamba kabla ya COVID-19, tulikuwa tukifanya hivyo.” Lakini anatambua kuwa kila kitu ni kigumu zaidi sasa na washiriki wa kikundi hawawezi kulipa ada ya kila wiki.

CARE inawasiliana na vikundi kusaidia shughuli zao na kuwasaidia kuzuia kuenea kwa COVID-19. Shirika pia lilitoa vifaa vya bustani na vifaa kwa ajili ya ufugaji wa wanyama.

Eudes Hougbenou anafanya kazi katika shirika la CARE Benin-Togo. Anasema, “Wanawake na watoto ndio watu walioathirika zaidi na janga hili. Wana uwezo mzuri wa kuhamasisha wanafamilia na wenzao juu ya hatua za kuzuia.”

Anaongeza, “Uamuzi huu unahisiwa zaidi ndani ya kaya zao. Wanandoa lazima wafahamu juu ya usimamizi bora wa familia — chakula, kulea watoto.”

Barakoa zimevaliwa, viti vimewekwa vizuri, wanawake katika kikundi cha Mignomidé wamekusanyika Jumatano hii huko Dangbo. Wanajitahidi kuchukua tahadhari zinazohitajika ili kujilinda wenyewe na familia zao kutokana na COVID-19: “Lazima tukae katika umbali wa mita moja kutoka kwa wengine, tuvae barakoa, na kunawa mikono mara kwa mara kwa maji na sabuni.” Mawaidha haya ni sehemu ya kawaida ya mikutano yao ya kila wiki.

Wanaanzisha pia biashara mpya ya kutengeneza vifaa vya kufua kwa mikono vya bei rahisi. Wakikabiliwa na kiwango cha COVID-19, vikundi vya wanawake wa vijijini wanataka kufaidika na mikopo midogo midogo ya biashara ambayo inawaruhusu kuwekeza katika shughuli zao za kujiongezea kipato. Hii itawasaidia kukabiliana na matokeo ya janga hili.

Rasilimali hii imeandaliwa kwa msaada wa kifedha kutoka kwa serikali ya Canada uliotolewa kupitia Global Affairs Canada.