Enos Lufungulo | Aprili 30, 2018
Penina Mungure na binti zake wawili wakitembela bustani ya miche ya vanilla kuangalia kama kuna tatizo lolote. Hali ya hewa ni tulivu na angani hakuna mawingu na jua likikaribia kuzama. Bi. Mungure anasema, “Kulima vanilla kunahitaji usimamizi wa karibu, miche inahitaji kuangaliwa—angalau mara mbili kwa wiki.”
Bi. Mungure anaishi kijiji cha Kilala karibu na Mlima Meru kaskazini mwa Tanzania mkoani Arusha. Kwa kipindi cha nyuma tatizo kubwa kwake na kwa wazalishaji wengine wa vanilla ilikuwa ni kupata masoko ya uhakika. Lakini kwa miaka mitano iliyopita kampuni ya Natural Extracts Industries au NEI ilianza kununua vanilla kwa wazalishaji hawa.
Bi. Mungure anasema amekuwa akilima vanilla kwa miaka mingi kwa sababu zao hili halihitaji gharama kubwa kama mazao mengine. Anaelezea, “Kuzalisha vanilla hakuitaji hela nyingi kwa sababau zao hili halihitaji mbolea na viuatilifu vya viwandani.”
Anasema, tangu aanze kuzalisha vanilla magonjwa na wadudu hawajawahi kuvamia shamba lake. Akiwakuta wanyama au wadudu kama konokono hatumii sumu kuwauwa—anawatoa kwa mikono tu.
Bi. Mungure alianza kilimo cha mkataba na kampuni ya NEI mwaka 2013. Mbali na kumhakikishia masoko, kampuni imempa mafunzo ya mbinu bora za kuzalisha vanilla.
Wakulima wa vanilla wanauza punje na miche ya vanilla. Lakini wanapendelea kuuza punje kwa sababu kuuza miche kunapunguza kiwango cha uzalishaji. Bei ya kilo moja ya vanilla ni 60,000 mpaka 80,000 shilingi (sawa na dola 27-35). Wazalishaji pia wanaweza kuuza mche wa mita–mbili kwa shilingi 2,500 (sawa na dola 1.10).
Nickson Severine ni mtaalamu wa kilimo shirika la NEI. Anawatembela wakulima mashambani mwao angalau mara moja kwa mwezi kuona maendeleo yao shambani. Anasema, “Mara nyingi natoa elimu kwa wakulima jinsi ya kupanda vanilla kwa ufasaha katika vikundi na kwa mkulima mmoja mmoja.”
Bw. Severine anasema kuwa kampuni yake inawahakikishiwa wakulima masoko ya uhakika. Kampuni pia inawapatia wakulima vifaa vya kuhifadhia maji kwa ajili ya umwagiliaji, ambayo husaidia wakati wa mvua chache au ukame.
Philipo Sululu amekuwa akipanda vanilla Mkoani Arusha kwa miaka 10. Kama Bi. Mungure, ameingia mkataba na kampuni ya NEI baada ya kuhakikisha soko la uhakika. Amejifunza pia jinsi ya kupanda na kutunza vanilla kupitia mafunzo yaliyotolewa na kampuni.
Anasema makubaliano na kampuni yanamuwezesha yeye kuzalisha mbegu na miche mingi ya vanilla kuliko alivyokuwa akifanya awali. Anasema, “Nitaendelea kuzalisha vanilla kwa sababu nina soko la uhakika linalonipa bei nzuri.”
Ijapokuwa kilimo cha mkataba kinawapatia wakulima hela zaidi, Bw. Sululu anasema kilimo hiki sio kilimo rahisi. Anaelezea, “Kupanda vanilla inahitaji muda na uangalizi wa shamba… na kubebesha vanilla kwenye fito kwa sababu vanilla inaota kwa kujisokota na kukwea juu.”
Anasema wakulima wengi katika kijiji sasa wanaanza kushawishika kuzalisha vanilla kwa sababu kuna masoko ya uhakika. Wakulima wanaingia mkataba na NEI kununua mazao yao kwa bei nzuri baada ya mavuno.
Mungure anasema, tangu aanze kilimo cha mkataba, uzalishaji wake kwa mwaka umeongezeka mara tatu kutoka 5-15kg. Anapata shilingi 720,000 (sawa na dola 320).
Mbali na kuzalisha vanilla, Bi. Mungure pia anafuga kuku. Anatumia kipato anachopata kwa kuuza Vanilla kukuza mradi wake wa kuku. Anatumia hela kununua nguo kwa familia yake, umeme na maji.
Uniterra Tanzania inafanya kazi na wadau wa ndani katika sekta ya matunda, mbogamboga na utalii kuwasaidia wanawake wadogo na vijana kupata huduma za kiuchumi. Uniterra imewezesha uandishi wa simulizi hili. Uniterra inapokea msaada kutoka serikali ya Canada, inayotolewa kupitia Global Affairs Canada, www.international.gc.ca. Jifunze zaidi kuhusu Uniterra Tanzania katika mtandao wa Facebook katika tovutit: facebook.com/wusctanzania